Sunday, February 17, 2013

UTENZI WA K ATIBA MPYA 001-200



UTENZI WAKATIBA MPYA  TANZANIA

UKMT 001-200

Utangulizi

Awali namshukuru,
Kunifanya mtu huru,
NIsiuzwe kwa ndururu,
Mtumwa nikabakia.

Namshukuru Rahimu,
Kwa kunigea kalamu,
Akanipa ualimu,
Maisha kuyaelewa.

Namshukuru Ghafuru,
Kwa kutonipa uzuru,
Katiba yetu kuzuru,
Na mimi kuibadili.

Utenzi nauandika,
Ili yangu kusikika,
Katiba ninayotaka,
Na ninayoitarajia.

Iwe inaeleweka,
Hakuna niliposhika,
Wala kundini kuwekwa,
Ila nilipoanzia.

Katikati nabakia,
Kwa yafaayo Tanzania,
Upande kutoegemea,
Ila kwa wasionielewa.


1.
WAKATI huwa wafika,
Watu wakaerevuka,
Wakahoji mamlaka,
Kwa vitendo na tabia.

2.
Mamlaka huwekeka,
Kwa chama kuchagulika,
Katiba inavyotaka,
Mshindi akatawala.

3.
Ila bado mamlaka,
Wananchi watayashika,
Kwa wao hukopesheka,
Ili kazi kuifanza.

4.
Huwa yote madaraka,
Watawaliwa washika,
Na muda wanapotaka,
Walioko huondoa.

5.
Katiba inayofaa,
Na dira itaanzia,
Ikaichora ruia,
Wapi tunaelekea.

6.
Njia tukishaamua,
Rahisi kuifatia,
Tasihili kuingia,
Haraka yakafanzika.

7.
Tunataka Tanzania,
Afrika ya kung'aa,
Isiyonayo udhia,
Kwingine tunaojionea.

8.
Umoja kuzungumzia,
Wote tukakubalia,
Vipi inavyotakiwa,
Nchi kuisimamia.

9.
Na tunaowachagua,
Vibarua kujijua,
Kazi wakiichezea,
Wajue twawatimua.

10.
Kanuni wakifulia,
Na sheria kuchezea,
Kortini wataingia,
Na kinga kuondolewa.

11.
Tunataka Tanzania,
Ya uchumi wa kukua,
Serikali nyenzo kuwa,
Ili watu kwendelea.

12.
Kikwazo inapokuwa,
Lazima kuondolewa,
Pasina ya kungojea,
Miaka wanayopewa.

13.
Kura wataitishia,
Ya imani kuridhia,
Watu wakiikataa,
Joho letu kulivua.

14.
Tunataka Tanzania,
Itakayotujalia,
Kila koo kupatiwa,
Nyumba bora ilokuwa.

15.
Vijijini kuanzia,
Kunakonukia balaa,
Watu wanakougua,
Kwa manyata kukalia.

16.
Tunataka Tanzania,
Hifadhi inayojua,
Ikazitunga sheria,
Ufujaji kukataa.

17.
Mahaini watakuwa,
Hifadhi wanaochezea,
Wakasagwa na kupewa,
Kazii kwenda tumikia.

18.
Tunataka Tanzania,
Maji isiyoishiwa,
Yakatiririka mwaa,
Kila nyumba kuingia.

19.
Tunataka Tanzania,
Ya umeme kusambaa,
Kila kaya kupatiwa,
Isiwe kwetu sanaa.

20.
Tunataka Tanzania,
Mazingira kuenziwa,
Mbadala kutumia,
Kwazo kuni na mkaa.

21.
Gasi tunayochimbua,
Mitaroni ikatiwa,
Kwenye nyumba kuingia,
Mjini na vijijini pia.

22.
Tunataka Tanzania,
Inayotujali afya,
Gharama kusaidiwa,
Utotoni kuanzia.


23.
Gharama zikaachiwa,
Ngumu zisizowawia,
Maskini Tanzania,
Nao wakajisikia.

24.
Mifuko iliyokuwa,
Utashi kuongezewa,
Siasa kuondolewa,
Uyakini kuwaniwa.

25.
Kiukweli watakiwa,
Huduma zao kutoa,
Wasiifanye nazaa,
Wakaja kuwa udhia.

26.
Mfano uwe Ulaya,
Uingereza kwangalia,
Mfuko uliotulia,
Huduma unazitoa.

27.
Wazee kuangaliwa,
Lazima kuwatajia,
Pasipo hilo kutiwa,
Tutakuja kulaniwa.

28.
Si wachache kwangaliwa,
Wengine kusahauliwa,
Kusutwa kukafatia,
Aibu tukaingia.

29.
Mzee ahitajia,
Umma kumuangalia,
Pasina kupendelea,
Cheo alichojaliwa.

30.
Wote sawa tuakuwa,
Kikatiba kwangaliwa,
Hili tukilifikia,
Nchi pepo itakuwa.

31.
Hili nalipigania.
Kwani nami najongea,
Nani ataniangalia,
Kama sio Tanzania?


32.
Madhumuni nayo nia,
Kuijenga Tanzania,
Karne ikatimia,
Bila cha kuongezea.


33.
Mfano yetu ikawa,
Katiba kwenye dunia,
Hadi nje ikang'aa,
Wakadhania ni jua.

34.
Sayari nyingine pia,
Na sisi zikavutiwa,
Huko wanakotokea,
Wakafata Tanzania.

35.
Vizuri tulianzia,
Mwalimu kutuongoa,
Umoja ukaenea,
Na amani kuivua.

36.
Nyuma waliofatia,
Mwinyi alijisemea,
Vichuguu tutakuwa,
Au sivyo ilivyokuwa ?

37.
Zimepishana tabia,
Uwezo umefifia,
Mfano aliyekuwa,
Laiki hajatokea.

38.
Enziye waliokuwa,
Mie wote nahofia,
Kama ningelijaliwa,
Cheo ningewazuia.

39.
Kwa mapambo wanafaa,
Si vitendo kuvijua,
Hawanayo nadharia,
Fedha waabudu sana.

40.
Wameshindwa kujijua,
Moja kubwa kuchagua,
Nafasi wanayopewa,
Mengi budi kuachia.

41.
Mlobaki nawambia,
Hili mkilitambua,
Uongozi ni ridhaa,
Wafaa kuheshimiwa.

42.
Na anayeulilia,
Budi kujipambanua,
Sio kwa kuumbilia,
Ila haki kutambua!

43.
Haya atakayezua,
Ubora atajaliwa,
Chini akatuondoa,
Hadi juu kufikia.

44.
Wengine tukiachia,
Tunaenda kufulia,
Hata tulichojaliwa,
Kitakuja kupotea!

45.
Ila hapa Afrika,
Mtindo umeshazuka,
Watawala wanataka,
Kuyatwaa mamlaka.

46.
Kutawala wanataka,
Si uongozi kuwika,
Hata kama wamechoka,
Nafasi huililia.

47.
Ndio maana twataka,
Katiba inayotamka,
Waziwazi kuyaweka,
Mianya ikaondoa.

48.
Hali yao kuijua,
Toka walipotokea,
Wafika ipi hatua,
Na kama wanaridhia.

49.
Kipimo wakikijua,
Na majibu kutambua,
Maamuzi huamua,
Mikakati kuibua.

50.
Mkataba kwangaliwa,
Hilo mojawapo huwa,
Wakafanya kurejea,
Upya ukapitiwa.

51.
Mazingira wakijua,
Si zamani yalokuwa,
Ndipo wanapomua,
Watu waweza kataa!

52.
Ukisoma historia,
Kasoro utaijua,
Katiba ya Tanzania,
Ya wananchi haijawa.

53.
Mkoloni katwachia,
Na yake aliyotia,
Vyake akajilindia,
Sio sisi kutufaa!

54.
Vingi ukiviangalia,
Ukoloni vyanukia,
Ila juu walokuwa,
Harufu haisumbui ?

55.
La hasha, ninakataa,
Vizuri waisikia,
Ila kinachotokea,
Harufu waizoea.

56.
Utamu unakolea,
Ubwana kuutumia,
Hivyo wakiviondoa,
Kawaida watakuwa.

57.
Hali juu watakiwa,
Ya wananchi wao kuwa,
Bila ya kuzingatia,
Katiba waikosea!

58.
Katiba waikosea,
Pamwe kupu'za sheria,
Mengi tunayatambua,
Wananchi wadhulumiwa.


59.
Wananchi wadhulumiwa,
Wao juu kutokuwa,
Watumwa si 'tumikiwa,
Wakuwa kuwalimia!

60.
Katiba yajitambua,
Sio juu walokuwa,
Wananchi kusimamia,
Wao ndio watakiwa!

61.
Vingine haya yakiwa,
Uporaji watokea,
Ni mkubwa uharamia,
Jinai tupu ikawa.

62.
Wakati wa Ujamaa,
Mengi yalifanania,
Mabnepari Tanzania,
Hali nyuma ya pazi!

63.
Ubepari kuingia,
Na ujamaa kuvia,
Hali mpya twazua,
Twatakiwa kulijua!

64.
Chama kilichoyatia,
Yatakiwa ondolewa,
Umoja wingi ukawa,
Na usawa kutetea!

65.
Ukabila wa kichama
Siasa sasa zafuma,
Ni balaa si neema,
Ila hatujalijua.

66.
Haki kuipigania,
Sasa lengo latakiwa,
Za halali kutumia,
Tenzi za demokrasia!

67.
Ni adui atakuwa,
Muua demokrasia,
Popote anapokuwa,
Lazima kumuondoa!



68.
Tunaitaka ruia,
Au visheni kujua,
Ni ramani inakuwa,
Mlango wa kujipitia.

69.
Budi hapa kuamua,
Kama bepari tutakuwa,
Nguo zote kuzivua,
Tusibakie na haya.

70.
Au kidogo kutia,
Machache yakabakia,
Wenye utu kuridhia,
Ubepari-ujamaa!

71.
Kila kitu kukitwaa,
Ubepari Tanzania,
Nchi tutaizingua,
Mhemuko ikatiwa!

72.
Yapo yakuangalia,
Na kisha kuyachagua,
Yale yanayotufaa,
Vyema tukayatumia.

73.
Mathalani tunajua,
Uzalishaji unafaa,
Watu wetu kuachiwa,
Nchi itaendelea!

74.
Biashara ni balaa,
Ovyo tunapoachiwa,
Kuchuma hupigania,
Hata watu tukaua.

75.
Huduma zinatufaa,
Pia kuziangalia,
Za kibepari zikiwa,
Kuna watakaofulia.

76.
Sera ninayolilia,
Mchanganyiko ikawa,
Mengi inachanganyia,
Kila bora kuchukua.



77.
Mbali tungelianzia,
Viongozi kuchungua,
Wazazi waliokuwa,
Na kama wametimia.

78.
Haramu wakiingia,
Wataileta nazaa,
Watu wakatunyanyua,
Badala ya chini kukaa.

79.
Kiongozi Tanzania,
Awe na historia,
Si tu ya kupitia,
Kwenye chama cha siasa.

80.
Inatupasa kujua,
Kizazi kilikoanzia,
Ukoo yake tabia,
Nayo wazi pia kuwa.

81.
Kuna asili udhia,
Kwa vita zinazaliwa,
Hitler aliyekuwa,
Kama huko katokea.

82.
Utoto ulivyokuwa,
Wenzie akiwafanyia,
Kama babe lilikuwa,
Bado litaendelea.

83.
Wazazi twapasa pia,
Na wao kuwatambua,
Bishara yake tabia,
Ndiko inakoanzia.

84.
Na jirani kutwambia,
kama kweli ilikuwa,
Wako wengi wakuzua,
Senti wakishazipewa.

85.
Rais awa Tanzania,
Usafi anatakiwa,
Nyumbani akianzia,
Hadi kazini kwingia.

86.
Shuleni tukayajua,
Rekodi kutupatia,
Sifuri waliokuwa,
Tusije tukaridhia.

87.
Ujana tukachungua,
Jinsi alivyotumia,
Anasa aliyejaa,
Aweza akatulia ?

88.
Njia alizopitia,
Zote tupate kujua,
Salama zinapokuwa,
Hapo twaweza pumua.

89.
Fujo waliozoea,
Ukubwani hurejea,
Kama vichaa wakawa,
Matatani kututia.

90.
Wakati ukifikia,
Urais kugombea,
Ushauri nautoa,
Njia bora kutumia.

91.
Adili tungeanzia,
Mapema kujipandia,
Wote wamoja tukawa,
kwenye hili kuamua.

92.
Je, rais maridhia,
Ni yupi atayekuwa,
Wajaao ukichaa,
Kabla mwaka kwingia?

93.
Ovyo kujipayukia,
Wao kiguu na njia,
Watu wakatumia,
Promosheni kuzua?

94.
Au kimya wa kukaa,
Kazi wanajifanyia,
Pasina kupendelea,
Kwao walikozaliwa?


95.
Nyuma wasosukumiwa,
Na ajenda walojaa,
Wataka kumtumia,
Zaidi kufanikiwa?

96.
Nini amewafanyia,
Kwao anakotokea,
Si wa kuwakimbia,
Hadi mlo kurejea!

97.
Ajenda alyezua,
Kwao na kwa jirani pia,
Umoja wakaujua,
Na kuipiga hatua.

98.
Elimu waliyopewa,
Kisha wakaitumia,
Wakatunga nadharia,
Wengine kujisomea!

99.
Au waliofulia,
Katu wasiobukua,
Vijiwe wavikalia,
Wakaongeza ujuha?

100.
Kiakili kakomaa,
Na kazi anaijua,
Au yeye angojea,
Wengine kumfanzia?

101.
Awe anayeamua,
Pasina na kuchungua,
Au anayechimbua,
Kwa haki akaamua?

102.
Hasira anayejaa,
Ovyo kujitamkia,
Murua akapungua,
Na kasoro kumjaa?

103.
Au aliyetulia,
Tathmini aijua,
Achukuaye wasaa,
Kila kitu kupembua?



104.
Kwake anayetulia,
Sio kiguu na njia,
Yake yakitengemaa,
Ndio akajitokea?

105.
Nyuma asiyefatiwa,
Na hila waliojaa,
Nchi wakajiuzia,
Hali yeye asinzia?

106.
Anachukua wasaa,
Kujisomea sheria,
Japo amepotia,
Mbalimbali tasnia ?

107.
Katiba akaijua,
Kufumba na kufumbua,
Chenga kutoadhiriwa,
Kwani yote ayajua?

108.
Imani aliyejaa,
Si asiyejitambua,
Kama boya yeye kuwa,
Baharini aelea!

109.
Pande asiyeegemea,
Na mjini kazaliwa,
Huko kutopendelea,
Vijijini kuwafaa.

110.
Kabila alozaliwa,
Juu kutoinuliwa,
Kwa hasara ya jamia,
Ukiwa wakaingia.

111.
Dini asiyetumia,
Wala zisizomtumia,
Usawa kusimamia,
Mola akapendezewa!

112.
Uungu kutojitia,
Unyonge akauvaa,
Kisha akanyenyekea,
Hata wadogo wakiwa?



113.
Dola asiyetumia,
Watuwe ngeu kutia,
Na macho wakaugua,
Na viungo kulemaa.

114.
Askari kuwatumia,
Uhalifu kuzuia,
Sio kuwageuzia,
Mbwa walioibiwa!

115.
Rushwa asiyeachia,
Polisi kuwa hidaya,
Ikageuka kinyaa,
Na watu kuwachukiya.

116.
Mkuu anayejaliwa,
Polisi kumsikia,
Kisha wakamhofia,
Huruma asiyekuwa.

117.
Asiyependa udhia,
Na raia kupakaziwa,
Awezaye kupindua,
Kila kitu kipya kuwa.

118.
Mahakama mwenye nia,
Uhuru kuiachia,
Sio kuiingilia,
Yeye akajipendelea.

119.
Bunge la waheshimiwa,
Uhuru kuliachia,
Sio mbeleko kutiwa,
Wakawa waning'inia.

120.
Adili ninarejea,
Lazima kutangulia,
Hili sio la kwachia,
Muda ukayoyomea.

121.
Wapaswa Watanzania,
Ukweli kujivunia,
Uongo anayetumia,
Huyo tukamuumbua.

122.
Kama cheo alipewa,
Iwe budi kuachia,
Na vingine kuvuliwa,
Hadi uchi kubakia.

123.
Uwizi kwa Tanzania,
Waweza sana pungua,
Mfano juu kukiwa,
Cheoni kuondolewa.

124.
Hata wakisingiziwa,
Na uwizi kunukia,
Harufu itatufaa,
Mamlaka kuyatwaa.

125.
Ngono akishuhudiwa,
Mara moja kumwengua,
Kazi asijechafua,
Ya watu kuathiriwa?

126.
Mlevi hatatufaa,
Na uraibu wake pia,
Katu kutokaribia,
Ikulu kwenda kukaa.

127.
Kupimwa inatakiwa,
Akili tukazijua,
Wapo walio vichaa,
Tusije kuwaachia.

128.
Ovyo wanaokimbia,
Njiani kujiropokea,
Wasiwasi wanatia,
Kama hawajapungua.

129.
Kama hawajapungua,
Au hawajazidiwa,
Kushonana zimejaa,
Zinashindwa kupumua.

130.
Mheshimu familia,
Huyo ataka enziwa,
Na wana kumsaidia,
Watu wema kuja kuwa.


131.
Katiba inatakiwa,
Kwa ufupi kurejewa,
Ili yetu kuepua,
Yaliyoiva haswaa.

132.
Mifano tunaijua,
Huko Kenya na Zambia,
Zimbabwe wafatia,
Ghana tukamalizia.

133.
Mageuzi yatakiwa,
Wakati ukishawadia,
Mabadiliko kuzua,
Nchi yakaja okoa.

134.
Elimu kuinyanyua,
Daraja jipya ikawa,
Malengo tukayajua,
Na dira kufafanua.

135.
Uchumi ili kufaa,
Watakiwa kufuliwa,
Tayari ukishang'aa,
Njia sahihi kujua.

136.
Hamsini kutimia,
Ni aibu tena waa,
Umaskini kubakia,
Lazima kuondolewa.

137.
Ulaya wametangulia,
Amerika kufatia,
Uarabu wajitoa,
Na Asia wanakimbia.

138.
Afrika twabakia,
Indiketa kwangalia,
Sasa basi twaamua,
Lazima kujichochea.

139.
Tutumie kila njia,
Kwa katiba kuandaa,
Milango inayofungua,
Kuuondoa ufakiri.


140.
Ufakiri ni balaa,
Kwetu kutoruhusiwa,
Wapaswa kushambuliwa,
Bilkuli kuung'oa.

141.
Neema ikabakia,
Waafrika kujaliwa,
Tukaacha angaliwa,
Kama 'boi' tulokuwa.

142.
Heshima kujipatia,
Tuache kutegemea,
Yetu tukajifanzia,
Kwa akili kutumia.

143.
Rasilimali zajaa,
Hadi wanatuibia,
Laiti tukijijua,
Haya hayatatokea.

144.
Wataingia vichaa,
Vita kutuanzishia,
Kama ilivyokuwa,
Amerika Latinia.

145.
Na Vietnam pia,
Waasisi twawajua,
Ufaransa kaanzia,
Marekani kafatia.

146.
Vyema tukawaambaa,
Mchina kutusaidia,
Vitani kutoingia,
Kwa yasiyotusaidia.

147.
Mmarekani balaa,
Watu apenda tumia,
Na hapo usipomfaa,
Teke atakutupia.

146.
Dunia ya kuchagua,
Pande ipi kwegemea,
Zipo safi na balaa,
Yafaa kuzikimbia.

147.
Mugabe ametuusia,
Mashariki kwanglaia,
Rahisi tukavijua,
Na salama vilokuwa.

148.
Vinginevyo kuumia,
Kawaida itakuwa,
Pasiwe wa kumlilia,
Wala kupata fidia.

149.
Misingi inayotakiwa,
Uhuru kuutetea,
Kila mtu huru kuwa,
Pasina ya kudhulumiwa.

150.
Wito nawatangazia,
Wote wanaonisikia,
Taasisi kuvumbua,
Mafunzo bora kutoa.

151.
Ya mwalimu taasisi,
Iwe ndiyo muasisi,
Ikaanzia kwa kasi,
Insha zake kufunza.

152.
Za mwalimu nadharia,
Wana wakaandaliwa,
Mazuri wakayajua,
Na dhaifu kugundua.

153.
Ubepari twauvaa,
Ila twaona wapwaya,
Bado zeke nadharia,
Hazinaye kufichua.

154.
Mbio kutokimbilia,
Ubepari kutuoa,
Tutakuja lijutia,
Tukabakia wakiwa.

155.
Taratibu inafaa,
Mchanganyiko ukawa,
Ya mtu yasiyofaa,
Umma wote kuachiwa.

156.
Umma wasiyopembua,
Ukiritimba kujaa,
Hayo tukawaachia,
Binafsi kufanzia.

157.
Haki ikaangaliwa,
Kwa wote sawa ikawa,
Pasiwe wa kununua,
Wala wa kujiuzia.

158.
Usawa unatakiwa,
Wote tupate jaliwa,
Sio wakapendelewa,
Hao wanaowajua.

159.
Na sisi tukaonewa,
Pamwe na kusahauliwa,
Hadi tukajichukia,
Na kuibeza dunia.

160.
Wana tunaojizalia,
Tusije tukawagawa,
Wenyewe kujibagua,
Kikazuka kizaazaa.

161.
Nchi tukajijengea,
Kila mtu kuridhiwa,
Uhuru kutunukiwa,
Halali kujifanzia.

162.
Kama maua tukawa,
Kila aina twajaa,
Hali tofauti zawa,
Rangi tulizojaliwa.

163.
Sheria inatakiwa,
Juu ya wote ikawa,
Kwa rais na raia,
Hapo wote kuwa sawa.

166.
Zama zajiondokea,
Mkuu juu kwachiwa,
Yake akajifanzia,
Hata yaliyo udhia.

167.
Rais akiachiwa,
Akawa juu ya sheria,
Twaweza pata kichaa,
Kama Amin akawa.

168.
Ikulu wakaingia,
Kitu wasiosikia,
Wakilindwa na sheria,
Wengi tutagugumia.

169.
Mawaziri watakwea,
Kuta wasizopitia,
Kwa kuwa wajitanua,
Rais kawachagua.

170.
Makamanda nao pia,
Kiburi kitawajaa,
Kwani wamechaguliwa,
Na kiranja alokuwa.

171.
Kadhalika wa mikoa,
Jeuri watatumia,
Watu wakawaonea,
Na vituko kuvizua.

172.
Aidha kwenye wilaya,
Yao watashupalia,
Na huku wakijitia,
Juu inawatumia.

173.
Usawa unatakiwa,
Ikatawala sheria,
Kila mtu akijua,
Akikosa huumia.

174.
Pasiwe wa kuumia,
Na katu wasioumia,
Neema wanaopewa,
Na mkuu aliyekuwa.

175.
Haki kuipigania,
Katiba inatakiwa,
Asiwe wa kuminyiwa,
Na kisha akaonewa.

176.
Pasiwe wa kununua,
Kisha akajiuzia,
Twaona yanayotokea,
Uhasama yanazua.

177.
Kibao hugeuziwa,
Haki apaswaye pewa,
Mwenye fedha akitoa,
Yeye akazawadiwa.

178.
Hilo budi kukataa,
Lisiachwe kwendelea,
Itavia Tanzania,
Hadi vita kuingia.

179.
Haki anayechezea,
Katu kutovumiliwa,
Maporini kutupiwa,
Bure akatumikia.

180.
Kama vile Serbia,
Inavyofaa Russia,
Unakofichwa udhia,
Wananchi salama kuwa.

181.
Rais kaelemewa,
Mamlaka kuyagawa,
Hili jambo la kufaa,
Vikwazo tutaondoa.

182.
Mkuu akichagua,
Wa polisi alokuwa,
Hatotii Tanzania,
Yeye kumnyenyekea!

183.
Mawaziri watakiwa,
Kazi wakajiombea,
Wabunge wasiokuwa,
Ila sifa walokuwa.

184.
Hawa wakiendelea,
Majimbo mengi kupwaya,
Yatakayoendelea,
Na waziri yalokuwa.

185.
Na wakuu wa mkoa,
Hebu tuache hekaya,
Sasa tumeshafulia,
Kuchaguliwa ni njia.

186.
Kuchagulwa ni njia,
Si rais kuteua,
Watu wakatupatia,
Na uchungu wasokuwa.

187.
Vyama pia vyatakiwa,
Mikoa kuigombea,
Ushindani vikatia,
Ustawi ukakua.

188.
Ninatamani pia,
Kuwa bunge la mkoa,
Waziri likachagua,
Mkuu atakayekuwa.

189.
Mkoa huru ukiwa,
Nchi itachachamaa,
Ushindani ukakuwa,
Mikoa kujinyanyua.

190.
Ya Mtwara kutokea,
Ni vigumu itakuwa,
kwa kuwa yao wapewa,
Na vyetu watuwekea.

191.
Mabunge wayalilia,
Pengine kwa kutojua,
Mawili tu kupatiwa,
Mimii ninaongezea...

192.
Mabunge yanatakiwa,
Thelathini ya mkoa,
Kisha yakafatia,
Mawili ya kitaifa.

193.
Ya mkoa kuzungumzia,
Yanyohusu mkoa,
Bila muda kupotea,
Na porojo kuzagaa.

194.
Ya taifa yatakuwa,
Mawili yaliyoshupaa,
Moja la kuchaguliwa,
Pasina wa kuteuwa.


195.
La pili la kuteua,
Makundi kwenye jamaa,
Maslahi kufatia,
Kwa karibu na ridhaa.

196.
Ya mikoa kutumia,
Muda mwingi na wasaa,
Ya taifa kwa masaa,
Ya kwao yakatimia.

197.
Hapo tukishafikia,
Itafungka Tanzania,
Kutakwisha kutambaa,
Tukaanza kutembea.

198.
Hatua ikafatia,
Mbio tuanze tumia,
Maendeleo kuzua,
Ya kweli yatayokuwa.

199.
Mahakama inatakiwa,
Huru itakayokuwa,
Mtu asiyoingilia,
Akazipinda sheria.

200.
Jaji mkuu Tanzania,
Asiwe wa kuteua,
Wengi wangechaguliwa,
Bunge Jaji kumchagua.


No comments:

Post a Comment