Sunday, February 17, 2013

UTENZI WA KATIBA 800-940


800.
Hakika hapa twapwaya,
Ila cha babu kikiwa,
Sasa kinachosahauliwa,
Na kingine kungojewa.
801.
Mavazi hatujaamua,
Na miaka yaishia,
Ni sanaa imekuwa,
Ndee-nani ayajua!
802.
Inacheka historia,
Kigugumizi kikiwa,
Wapi tulipopotea,
Ila usanii kuvaa?
803.
Thamani inatakiwa,
Ya mzawa Tanzania,
Vipi Mwadui akawa,
Sawa na kusikokuwa.
804.
Na thamani ni uchumi,
Ardhini uliokuwa,
Huo ukichanganuliwa,
Mwananchi kuongezewa.
805.
Ya Wazungu na Asia,
Mabwana wakaja kuwa,
Hapo wasingefikia,
Na thamani tungekuwa.
806.
Saluti tungepigiwa,
Kama kwa wenye kujua,
Waarabu maridhia,
Sana wanaheshimiwa.
807.
Qatar ukiingia,
Na Dubai nako pia,
Hili utaligundua,
Wivu ukakuingia.

808.
Imeshazuka tabia,
Wakubwa kujifanzia,
Bila sisi kuyajua,
Na kisha kudharauliwa.
809.
Na kisha kudahauliwa,
Na matusi kutupiwa,
Hili ninawaambia,
Kubaya twaelekea.
810.
Mtu hauwezi kuwa,
Pasina na watu kuwa,
Ukitaka  kulijua,
Porini ukitupiwa.
811.
Wakubwa mngerejea,
Nafsi kuziangalia,
Ukubwa sio kupaa,
Au malaika kuwa.
812.
Ni watu wa kujijua,
Ndio nchi hujaliwa,
Ila wasiojitambua,
Kwao nchi huangamia.
813.
Mtakatifu hujawa,
Hadi unapojifia,
Ulimi ukiamua,
Unaweza kuchafua.
814.
Unaweza kuchafua,
Na motoni kwenda kaa,
Mazuri uliyodhania,
Yote yakawa kinyaa.
815.
Ni chafu historia,
Ya nchi hii Tanzania,
Ushiriki ni tanzia,
Kuzikwa ulishajifia.
816.
Mchezo wakichezewa,
Enzi zilotangulia,
Pahala wakaishia,
Vijiji vikawa baa!

817.
Kinyume kiangalia,
Yahudi wametimia,
Vyao wamevinyanyua,
Kitega uchumi kuwa.
818.
Sisi tuliochezea,
Shilingi tukaachia,
Chooni ikaingia,
Twawa ni wa kufulia.
829.
Tulichokikosea,
Raia tulihadaa,
Kwa king'enge kwishia:
'Manipulation' hatua.
821.
Tiba hatukuijua,
Therapy kufafanuliwa,
Tukaganga yetu nia,
Na nyufa kuzitumia.
822.
Taarifa nayo pia,
Hiyo hatukuifikia,
Kwani tulipoishia,
Hatujui ni 'Informing'.
823.
Leo ukitembelea,
Vijiji vya Tanzania,
Ufahamu wafulia,
Ila tu yao kujua.
824.
Kwao ni giza dunia,
Mawasiiano sanaa,
Kwa simu isipokuwa,
Na mnara palokuwa.
825.
Yao wakaongelea,
Na umbeya kuupokea,
Ila habari kujua,
Bado wanatahiniwa.
826.
Ushauri umevia,
Nani watakusikia,
Imeshazuka tabia,
Kila kitu wanajua.

827.
Wazo ukiwaachia,
Haraka watakuibia,
Mkia wakauchukua,
kishwa wakakuachia.
828.
Nusunusu huyazua,
Ndio kufa kuwa kawa,
Nam sintosikitikia,
Pasi katiba kuwa dawa.
829.
Kwingine tukachagua,
Kwenda kubembelezea,
Kura tukajiombea,
Ndiko kulikoendelea.
830.
Na mtu wasiyekuwa,
Au mwoga aliyekuwa,
Nyuma wakawa  mkia,
Ya kwendelea Tanzania.
831.
Fuo zinazotakiwa,
Ni ubia kulelewa,
Pamoja wakayazua,
Nchi yatayonyanyua.
832.
Hapo wakishafikia,
Mamlaka kukaimiwa,
Huru ikiwa mikoa,
kasi yetu ya kupaa.
832.
Ushindani ukiingia,
Wa kweli uliokuwa,
Wavivu watajijua,
Wenyewe kujiondoa.
833.
Wabebwa watang'aamua,
Ngazi wakaziachia,
Barubaru wakatwaa,
Kilele kuelekea.
834.
Hatua itafikiwa,
Umma ukajitanua,
Mamlaka kuyagawa,
Washike Watanzania.

835.
Hapo watakaobakia,
Si rushwa waliotoa,
Ila wanaojijua,
Na wajibu kutimia.
836.
Mabaraza yatakiwa,
Kwa kuanzia wilaya,
Wakazi wakachagua,
Rasimu kuzungumzia.
837.
Kazi wakaichambua,
Tume itayomalizia,
Makosa wakafichua,
Mazuri wakasifia.
838.
Hapo wakimalizia,
Juu kupelekewa,
Baraza la kimkoa,
Nalo likazungumzia.
839.
Ubora yakaongezewa,
Chini yaliyofikiriwa,
Zaidi ikanolewa,
Katiba ya Tanzania.
840.
Ni heri ya kuchelewa,
Kuliko tukakimbia,
Mkenge kuparamia,
Kesho tukaja kulia.
841.
Ikitokea mkoa,
Taifa itangia,
Baraza sasa kukaa,
Wawakilishi Tanzania.
842.
Hao watayachambua,
Chini yaliyotokea,
Na mapengo kuondoa,
Katiba ikatimia.
843.
Wasemaji watakiwa,
Wa nje kuja ingia,
Wakasikiiza raia,
Yao wakizungumzia.
844.
Na wao wakachangia,
Udhaifu kuondoa,
Kisha mengi kuyatia,
Katiba mnofu kupewa.
845.
Njia kutozizuia,
Wakuu waliokuwa,
Viwanjani kutumia,
Helikopta kwingia.
846.
Hizo Ikulu kutua,
Au wanakokalia,
Watu kutowasumbua,
Kwa ving'ora vya udhia.
847.
Wagonjwa wakabakia,
Na wazazi nao pia,
Njia zetu kuwafaa,
Na sio kucheleweshwa.
848.
Hatima naitumia,
Wanatume kuusia,
Uongozi kwangalia,
Kupata unaofaa.
849.
Watumie zote njia,
Katibani hilo kuwa,
Mikakati kuizua,
Iwezayo kutufaa.
850.
Mfumo kufikiria,
Safi sana ulokuwa,
Uwezao kuchagua,
Salama anayekuwa.
851.
Wenye uchu na tamaa,
Mapema tukawajua,
Na wao mabwana pia,
Mafichoni kutokuwa.
852.
Watu wanaonunua,
Ili kuwatumikia,
Wao wakijidhania,
Ndio aali wafaa.

853.
Wao wakajidhania,
Ndio aali wafaa,
Wengine wana madoa,
Usafi wakajitia!
854.
Ukwasi wanaonuka,
Kwa vyanzo viso hakika,
Hao bora kufunika,
Kwenye teuzi kutoa.
855.
Bwana wawili wakiwa,
Atashindwa kujigawa,
Nchi akaionea,
Na kuinyonya balaa.
856.
Mchapakazi kwangalia,
Mageuzi wa kuzua,
Chini asiyetulia,
Raia kutumikia.
857.
Hiyo akatunukiwa,
Kichama kupigania,
Uongozi kugombea,
Azidi kutumikia.
858.
Usitupe katiba we,
Viongozi mamlukiwe,
Kama wapo wazobowe,
Safu zikasafishika.
859.
Kisha usitujalie,
Madaraka wayatwawe,
Raia tusiumie,
Hapa kwetu Tanzania.
860.
Bwana utuhurumie,
Wa kuteseka tusiwe,
Viongozi sitwachie,
Wanaokuwa fisadi.
861.
Marafiki wa mahoka,
Jamaa hawa dhihaka,
Makubwa wanayataka,
Ili wao kujaliwa.

862.
Wanaifanza hadaa,
Nchi mema waitakia,
Na watu watainua,
Hali bora kuijua.
863.
Uzaini huishia,
Yao kujikusanyia,
Sisi tunapojifia,
Hilo halitawasumbua.
864.
Wageuze ni maboga,
Tembo kwenda kukanyaga,
Si sumu ya kuwabwaga,
Uhai ukakimbia.
865.
Usitupe viongozi,
Waliyo nao mapenzi,
Wamashoga viongozi,
Kaumu Lutu kuambaa!
866.
Wazungu waabuduo,
Na walokuwa kama hao,
Tuwe tuwatapikao,
Maslahi yasipokuwa.
867.
Ya kwao tukayazoa,
Wawe wabakiao,
Ni rafiki wa kutua,
Kesho kujiondokea.
868.
Waabuduo Wazungu!
Yakini tangu na tangu,
Tumkurubie Mungu
Hilo akaliondoa.
869.
Badala ya kufungulia,
Huu mkubwa ukiwa,
Viongozi kama hawa,
Hawafai kuongoza.
870.
Vijiji wasiojali!
Ila kwao kwenye mali,
Ifike ardhilhali,
Heri nasi hawajawa!

871.
Uzeeni twaumia
Ahadi walizotoa,
Tiaifa tukidhania,
Litakuja twangalia.
872.
Wote nao twapishana,
Na mabega kugusana,
Hawaioni hiana,
Wajifanya kutojua.
873.
Kwalo hawana ujuzi,
Vijana kukosa kazi,
Ndio duni viongozi,
Huona yao ya maana.
874.
Wameijaa hadaa,
Kuwazaini raia,
Ahadi kama ruia,
Kitu zisizotufaa.
875.
Hii ni ya umma dua,
Muumba wetu sikia,
Kitu wasiosaidia,
Hwajawa viongozi.
876.
Rushwa waikubalia,
Na kutooana kinyaa,
Wote hivyo weshakuwa,
Paka kengele agoma!
877.
Nchi watajiuzia,
Tusipowaangalia,
Tutakuja amia,
Wageni weshachukua.
878.
Na wezi wenye ubia,
Nchi watatuulia,
Kidogo tunachopewa,
Wao wakakichukua.
879.
Imani inawajaa,
Kwa yao kukubaliwa,
Kuna wanalosaidiwa,
Hadi wakaaminiwa?
880.
Ukweli wanaojua,
Nje hawatautoa,
Porojo watazitia,
Wajua kupotezea!
881.
Danganya wakomalia,
Sera kutozungumzia,
Sera wakajifichia,
Wananchi kutokujua.
882.
Mbegu tuliozotia,
Mola anazijalia,
Zimeanza kuchanua,
Uongo kuja jitenga.
883.
Chini chini kupitia,
Kwa hao wanatania,
Yao wakaysikia,
Umma upate ambiwa.
884.
Siri kitu haijawa,
Umma inayochezea,
Na mali kuzitumia,
Halali isivyokuwa.
885.
Siri zinazotakiwa,
Ni za njia kugundua,
Tunazoweza tumia,
Taifa kulinyanyua.
886.
Siri ya kujifichia,
Ya umma yaliyokuwa,
Yenu mkajifanyia,
Hiyo haitakubaliwa.
887.
Siri miradi kuua,
Nchi kutokuendelea,
Ni uhaini inakuwa,
Budi zikafichuliwa.
888.
Siri ya kujiuzia,
Vya kwenu visivyokuwa,
Mfukoni mkatia,
Halali haitakuwa.

889.
Ovyo wanatutendea,
Ufakiri kututia,
Na nusura kutojua,
Sio sifa ni laana.
890.
Waumizao raia,
Sababu kutoijua,
Kisha kunyimwa fidia,
Yafaa kuliangalia.
891.
Wakubwa walitambua,
Ila wajinyamazia,
Halali tukadhania,
Udhia kuvumilia.
892.
Dhuluma waliojaa!
Wanaabudu dunia,
Sisi wakatudhania,
Ndio tulio vichaa?
893.
Katiba ya Tanzania,
Pupa kuiangalia,
Kisha kanuni kutoa,
Ratiba kuandaliwa.
894.
Mtu asipofatia,
Ikawa yamuondoa,
Mbioni anakoingia,
Pasina ya kuruhusiwa.
895.
Watu wanaochezea,
Hao ni kuwafagia,
Pembeni wakazolewa,
Kwenye kapu la historia.
896.
Kama wao walokuwa,
Pembeni waliishia,
Ikajifia tamaa,
Na magonjwa kuwavaa.
897.
Wabaya wakitokea,
Mkoloni bora kuwa,
Hao ni wa kuwaondoa,
Kwa kura kuitumia.

898.
Mbele wanaojita,
Wabaya kuwatetea,
Tena kuwarejelea,
Hukumu tukaijua.
899.
Vya kwetu vinajinywea,
Kitu kutoambulia,
Chungu chetu kikajaa,
Na afueni kujua.
900.
Wasiojua kuchuma
Rushwa kwao ndio noma,
Wakaikosa huruma
Kuwapa Watanznia.
901.
Ila hawawezi kazi,
Nje hawa kizuizi
Wakaishia uizi
Kama tunavyoyaona.
902.
wasioweza kuchuma!
Migodi kuisakama,
Huwageuka dhuluma,
Na wao wakafulia.
903.
Hao lazima kuchamba,
 Kwa tabia ya manamba,
Jalalani kuwasomba,
Tukaepuka balaa.
904.
Vito bure wauzao!
Wasifae watu wao,
Ni laana watakao,
Kuipata ni hedaya.
905.
kabla haijatumiwa,
Kila siku kuanzia,
nyuma ya tulipoishia,
Usitupe viongozi,
906.
Upya mambo waanzao!
Ndo hsara watupao,
Yesha kuwa marudio
Charama mpya ikawa.

907.
Miili hufa kwa ganzi,
Ni mikubwa udokozi,
Wanazidi majambazi,
Hasara wanaotia.
908.
Fedha waficha Uswizi!
Twabaki matumbo wazi,
Kisha zawa simulizi,
Hatua kutochukua.
909.
Demokrasia kukwama,
Sasa tunarudi nyuma,
kwa kujenga uhasama,
Na viranja kulemaa.
910.
Watumiao uchama,
Vitisho wakavikama,
Kuziepusha tuhuma,
Si kheri waliokuwa.
911.
Chuki wanajipandia,
Upendo ukapotea,
Hivi washindwa jionea,
Kwingine yanayotokea?
912.
Dini chini wawekao,
Juu kujiona wao
Ni hofu wanitiao,
Mwisho wetu nahofia.
913.
Imani wachezeao,
Na utume wanunuao,
Naogopa domo lao,
Kitanzi kisije kuwa.
914.
Dini ndogo zaachiwa,
Uhuru wa kuchagua,
Kubwa inapofikia,
Haziachi ingiliwa.
915.
Yakini kwenye imani,
Uhuru si yumkini,
Inapaswa kila dini,
Ya kwao wakaamua.
916.
Wanaopewa kofia,
Mlango kutopitia,
Wa mbele uliokuwa,
Waweza zusha nakama.
917.
Waumini wakijua,
Imani inachezewa,
Ndiyo hayo hutokea,
Mikoani yatokea.
918.
Dar sasa yaingia,
Ibada zikazuiwa,
Na wanaokataliwa,
Wakazidi kutetewa!
919.
Malaika hukimbia,
Mioto twajiwashia,
Petroli twang'ang'ania,
Mwishoe hutulipua.
920.
Tukinge na uzinifu!
Na mwingine udhaifu,
Tukaikimbia harufu,
Pale tunaposikia.
921.
Mabaya wanaoyafanza,
Hao ukawaangaza,
Kazi hawataiweza,
Watakwaza Tanzania.
922.
Muntakimu umbua,
Wewe ndiwe muamua,
Wengine wanajitia,
Kisasi haujakuwa!
923.
Wao kuwageukia,
Ubaya wakiizua,
Nchii hii kuchezea,
Afu yako twaiomba.
924.
Moyoni ukamvaa,
Kisha sumu kutoa,
Mema ukamtilia,
Aweze kututendea.
925.
Katiba  kutotwibia,
Haki zetu zilokuwa,
Kama ya sasa ikawa,
Yatoa kisha kutwaa.
926.
Twajua yakutarajia,
Muamuzi kiamua,
Hakuna cha kubakia,
Ila Baki kuamua.
927.
Anayetoa udhia,
Hasa kwa zao hadaa,
 Uzaini kuishia,
Salama tukabakia.
928.
Wafwasi kununuliwa,
Hakika hili nazaa,
Nini watachochagua,
Uoza isipokuwa ?
929.
Wote wanaoteuliwa,
Ni wenyewe wajifaa,
Na bwana kutumikia,
 Wala si raia kufaa.
930.
Uchungu hawajajua,
Mwana hawajamzaa,
Manyang'ayu karaha,
 Ja, Kenya kuwatania.
931.
Sasa kwetu waingia,
Vipi twawavumilia?
Mbepari mjamaa,
 kiongozi Tanzania?
932.
Ubepari waingia,
 Wazaini ujamaa,
Mizizi wajichimbia,
Juu waliokuwa.
933.
Ardhi kujiuzia,
Bakshishi wapatiwa,
Ubora wanaojitia,
Yetu kuonea haya.
934.
Imani kuwapotea,
 Utumwa wakajitia,
Hawa si wa kutufaa,
Ni watu wa kutumiwa.
935.
Pesa wanaotumia,
Watu kujinunulia,
Kisha wakachaguliwa,
Kwa hila kuitumia.
936.
Ni dhuluma na nazaa,
 Kutokuivumilia,
Wajanja wanaojitia,
Kumbe wajinga wajua.
937.
Kamba ni kuwaachia,
 Wenyewe kujinyongea,
Hauwezi kushangaa,
 Maana yao wajua.
938.
Wasiopenda kusoma,
Na daima maamuma,
Maamuzi kujitoma,
Huikosea kalima.
939.
Hao meli yao kuzama,
Hawawezi uadhama,
Wenye chuki na hasama,
 Huroga kuneemeka.
940.
Ni la kwao kwa kaida,
 Hawaileti faida,
Hata wakiwa makada,
Hai bora kuwazika.

No comments:

Post a Comment