Sunday, February 17, 2013

UTENZI WA K ATIBA MPYA 201-400


UKMT 201-400

201.
Wakiona anafaa,
Tiki watampatia,
Na kisha kuwaachia,
Wajuzi kumhudumia.

202.
Hata rais akiwa,
Mahakama juu kuwa,
Yake atapitishia,
Tu yanakoruhusiwa.

203.
Yeye hatapendelewa,
Wala akaogopewa,
Bali itakapokuwa,
Hatari inahofiwa.



204.
Hatari kuamuliwa,
Watu wote kuzijua,
katibani kuainiwa,
Waziwazi tukajua.

205.
Vyombo vyetu vya habari,
Vinayo kubwa safari,
Hasa vyenye majemadari,
Siasa wanaobwia.

206.
Hivi vingelitakiwa,
Na baraza kwangaliwa,
Uovu kutambuliwa,
Na wema kuzawadiwa.

207.
Na wanaovitumia,
Kamasi kujifutia,
Katu kutokuachiwa,
Wala wakaruhusiwa.

208.
Ni nguzo ya kitaifa,
Haikubaliki nyufa,
Huo mbaya wadhifa,
Hatari unavutia.

209.
Ajira inatakiwa,
Vizuri kufunuliwa,
Na ujira kupatiwa,
Utumwa usiotia.

210.
Vingine ukiachiwa,
Wengi watanunuliwa,
Rushwa wasioijua,
Hapo kazi kupatiwa.

211.
Serikali yatakiwa,
Mwongozo kuridhia,
Taarifa kuzitoa,
Bila ya kulazimishwa.

212.
Mswaada unachelewa,
Ruhusa unaotoa,
Waandishi kuingia,
Taarifa kupakua.



213.
Siri budi kuzijua,
Zipi zinazostahilia,
Zingine nyingi balaa,
Wananchi zinatuibia.

214.
Hii yetu Tanzania,
Dini haikujaliwa,
Ila tuliozaliwa,
Zetu tumejirithia.

215.
Hivyo hatutoridhia,
Imani kuzichezea,
Dini wanaotambua,
Katiba ya Muumini.

216.
Matangazo ya zinaa,
Hapa kwetu Tanzania,
Kwanini yaruhusiwa,
Yaongeza umalaya.

217.
Kondomu yanasifia,
Na ngono kuichochea,
Na tunachojipandia,
Ni kukithiri ukiwa.

218.
Na utamu waitia,
Kwa ladha na kunukia,
Hii nikiangalia,
Naona chambo kinakuwa.

219.
Mila tungezirejea,
Kiini kukiagua,
Ya wazungu tukilea,
Tutakuja kujutia.

220.
Walau wanaonewa,

Kulia waliokuwa,
Kushoto wakidhania,
Ndio wanapendelewa.

221.
Redio wachakachua,
Na mitabendi kuvia,
Ruhusa waililia,
Tivii wakataliwa.

222.
Kiini hawajakijua,
Ila udini wahofia,
Haya tungeangalia,
Usawa ukaenea.

223.
Auaye kuuawa,
Vingine haitakuwa,
Amri tulikwishapewa,
Msije kuipindua.

224.
Hata na huko Ulaya,
Uhalali waujua,
Kifo anayekusudia,
Kifo malipo hupewa.

225.
Kadhi haiwi halali,
Kumfanyia udhalili,
Wapewao kulhali,
Huyu wakamkamia.

226.
Uhuru wa kuabudu,
Jumlaye maabadu,
Budi kutia hadidu,
Mahakama si ridhaa!

227.
Mahakama yatakiwa,
Islamu kuwafaa,
Kuwanyima ni hadaa,
Shere mnawachezea.

228.
Katiba inatakiwa,
Hili ikalitambua,
Na ujanja kuzuia,
Waumini kufanziwa.

229.
Yao wakiikataa,
Ya sekula kutumia,
Na zote zinatakiwa,
Dola kuziangalia.

230.
Ubaba wa kujitia,
Unatakiwa kujifia,
Hakuna wana wakawa,
Mbelekoni kwenda tiwa.

231.
Watu wetu wamekua,
Na uhuru kuchagua,
Lile wanaloamua,
Kwanza likafikiriwa.

232.
Ila waliojaliwa,
Kweli wakishatambua,
Halafu wakafichua,
Hiari budi ikawa.

233.
Wingi wetu kuutia,
Katibani kuridhiwa,
Vyana tumevizua,
Budi kuvihudumia.

234.
Vijijini watakiwa,
Uzuri kuelezewa,
Vyama vingi kujaliwa,
Neema tutajaliwa.

235.
Hivi vitapigania,
Lilo bora kupatiwa,
Mmoja wa kuchezewa,
Tena hatajabakia.

236.
Vyama pia vyatakiwa,
Ustawi kuchangia,
Miradi wakafungua,
Kujenga yetu mikoa.

237.
Na anayewazuia,
Upinzani Tanzania,
Huyo ni wetu adawa,
Anafaa kuchukiwa.

238.
Upinzani wafungua,
Vile tulivyofungiwa,
Uono ukautoa,
Mbali unaofikia.

239.
Vijijini ukikua,
Vijiji havitavia,
Na huko kwa kuanzia,
Haki kuzipigania.


240.
Haki kuzipigania,
Vijiji vikapatiwa,
Bora waliojaliwa,
Viongozi wa kufaa.

241.
Si bora wa kukaa,
Kitu wasiotambua,
Miaka ikaishia,
Vilevile kubakia.

242.
Uongozi ninalia,
Chini ndiko watakiwa,
Vijiji kuviinua,
Hadhi bora kufikiwa.

243.
Vijiji vinaumia,
Toka Nyerere kutwachia,
Nani wa kuangalia,
Isipokuwa Katiba.

244.
Iliyo yajisemea,
Uwiano utakuwa,
Katika kuendelea,
Ila mengine yafanzwa.

245.
Haki yaegemea,
Miji kuipendelea,
Huduma huko zajaa,
Vijijini ni adimu.

246.
Kikomo tungekitoa,
Vya msingi kupatiwa,
Hilo litachochea,
Vijiji kuvifufua.

247.
Maji tarehe tukawa,
Sote tunaitambua,
Huko yatawafikia,
Ima fa ima ikawa.

248.
Umeme aidha pia,
Tarehe tukaijua,
Gizani kuwaondoa,
Kushindwa kutokubali.



249.
Zahanati za kufaa,
Mwisho kuukadiria,
Kila kijiji pakawa,
Tiba nao wanapewa.

250.
Shule nazo tukajua,
Kila hali zatimia,
Pasina kitu kuvia,
Wala kikakosekana.

251.
Barabara nazo njia,
Mkakati kuufua,
Wanavijiji wakawa,
Wao waziangalia.

252.
Wao waziangalia,
Lakini tukalipia,
Vyanzo vikalelewa,
Endelevu hilo kuwa.

253.
Masoko kuwajengea,
Na hadhi yaliyokuwa,
Wao wakajikodia,
Maduhuli kuingia.

254.
Na uongozi kupatiwa,
Msasa unaotiwa,
Elimu wakagawiwa,
Ubora wao kukuwa.

255.
Maarifa kuletewa,
Ujasiriamali kwanzia,
Njia wakazing'amua,
Ufukara kuuvua.

256.
Huku juu wamejaa,
Hawana la kujifanyia,
Nafasi waitumia,
Kuutembeza umbeya.

257.
Na uongo kuzua,
Wengine kupakazia,
Wakubwa wasio haya,
Wamejaa Tanzania.


258.
Wanashindwa kutambua,
Siku itajaingia,
Mseto kuandaliwa,
Wapi watachungulia?

259.
Chama kimoja udhia,
Mengi kimetuulia,
Hesabu nikiitoa,
Mbona wengi mtalia.

260.
Ushirika kimeua,
Na kushindwa kufufua,
Nini wanajivunia,
Maiti kilichokuwa ?

261.
Vijiji vimechakaa,
Hoi taabani vyawa,
Wasichana angalia,
Wazee utadhania?

262.
Maji wanayfukua,
Sio ya kufungulia,
Maili wanatembea,
Porini kuyafatia.

263.
Na wengine wanaliwa,
Na wanyama wenye njaa,
Hakuna wa kutetea,
Hili mara moja lishe.

264.
Moto wanaotumia,
Kuni za kupigania,
Kisha wakachuchumaa,
Hadi kuwaka dunia.

265.
Macho yanaugulia,
Hadi mekundu yakawa,
Uzee ukiingia,
Uchawi wanazuliwa.

266.
Makampuni waua,
Na kisha kujinunulia,
Ufisadi unapwaya,
Chini wanazimwagia.


267.
Halmashauri zapwaya,
Imara zilizokuwa,
Siasa zilipoingia,
Hewa zikaichafua.

268.
Miundo inatakiwa,
Ya vyama vingi kuzua,
Inayoyachangamkia,
Chama inayoyachukia.

269.
Mifumo inatakiwa,
Kuzua teknolojia,
Haki ikatutendea,
Sisi sote Tanzania.

270.
Wanachama kuwajua,
Muhimu teknolojia,
Simu ukizitumia,
Idadi mtaitambua.

271.
Sio wanaoishiwa,
Mamluki kutumia,
Dodoma kupakuliwa,
Mizigo ukadhania.

272.
Simu mkizitumia,
Wafu wenu kupungua,
Hisabu ikatimia,
Michango kwa kuitoa.

273.
Wenye simu wanajua,
Orodha kuiandaa,
Ujumbe wakautia,
Ada kuikumbushia.

274.
Wanachama wakatoa,
Za kwao mkatumia,
Na sio kutupunguzia,
Kidogo kilichokuwa.

275.
Kama SACCOS kuundiwa,
Watu wanapochangia,
Mikopo wakaachiwa,
Pasina riba kutia.



276.
Wanachoma watatoa,
Ili mkopo kupewa,
Ubahili kupungua,
Na nyodo zikapotea.

277.
Biashara mtazua,
Nzuri na ya kusifiwa,
Wafuasi kunyanyua,
Na vyam mkaviokoa.

278.
Benk Kuu Tanzania,
Kuwa huru yatakiwa,
Ikaweza kuamua,
Pasina kuingiliwa.

279.
Gavana kwa kuanzia,
Lazima kuchaguliwa,
Jina bunge kupatiwa,
Pamoja kumridhia.

280.
Hesabu akitimia,
Kura apate pigiwa,
Akitoka kidedea,
Fursa akaachiwa.

281.
Aweza nje tokea,
Kama kazi aijua,
Si lazima kuchukua,
Mzawa alo mbaya.

282.
Ajira atazitoa,
Wasaidizi kuchagua,
Malengo kujiwekea,
Si vyama kutuambia!

283.
Siasa imechafua,
Benki Kuu Tanzania,
Ufisadi twaujua
Ndiko ulikoanzia.

284.
Vyama vinaivamia,
Na bakuli wachukua,
Msaada kulilia,
Kwa yao si Tanzania.



285.
Na wakuu twaambiwa,
Huko wanaogopewa,
Mikopo wakiamua,
Upesi waruhusiwa.

286.
Marufuku ingekuwa,
Benki kuikaribia,
Wanasiasa Tanzania,
Mbali sana wakakaa.

287.
Kisha benki yatakiwa,
Ubunifu kukazia,
Njia ikazigundua,
Ufakiri kuuvaa.

288.
Budi kujali mzawa,
Na yake kuyaangalia,
Kwa sera zinazofaa,
Kipato kutuongezea.

289.
Kuchangamsha yatakiwa,
Benki inazoangalia,
Ili kujititimua,
Mikakati kuzindua.

290.
Mikakati kuzindua,
Mikopo ikatolewa,
Na dhamana wakapewa,
Hasara kutoingia.

291.
Kichocheo yatakiwa,
Benki Kuu kwetu kuwa,
Si mzgo kuchukua,
Kitu usiotufaa.

292.
Mbele yatakiwa kuwa,
Benki Kuu Tanzania,
Dira ikaangalia,
Na udhibiti kupea.

293.
Vyama kutokutegmewa,
Kazi hii kuingilia,
Benki kuu yatimia,
Ndio itakayoamua.

294.
Rahisi kwetu ikawa,
Chama tunapochagua,
Na kingine kuondoa,
Bila hazina kuibiwa.

295.
Maadui Tanzania,
Upya inatakiwa,
Sasa hivi kuwajua,
Kwa maadili kuzua.

296.
Tunao tunaojua,
Hao wa kihistoria,
Toka uhuru kupewa,
Kuwepo waendelea.

297.
Umaskini Tanzania,
Mradi umeshakuwa,
Watu wanachachamaa,
Unafugwa na wakubwa.

298.
Unafugwa Tanzania,
Ufukara kuwafaa,
Viztio wasosha njaa,
Mitambi kuitambia.

299.
Kama wangeliamua,
Ni rahisi kuuzoa,
Mbali kuufagilia,
Kwa hivi tulivyojaliwa.

300.
Ila eti wahofia,
Huru watu watakuwa,
Njaa wakishaondoa,
Hawawezi chaguliwa.

301.
Umma budi kuamua,
Walo bora kuchagua,
Bila ya kufikiria,
Chama wanachotokea.

302.
Ujinga tunahofia,
Hivi sasa warejea,
Katiba inatakiwa,
Hili ipate zuia.


303.
Kwa kuagiza sheria,
Mfuko kuzinduliwa,
Utakaoangalia,
Ujinga kutokusambaa.

304.
Mikakati itazua,
Itakayotungwa sheria,
Na watu wa kubobea,
Na wengineo raia.

305.
Kitu kinachotakiwa,
Ujinga kutoruhusiwa,
Shule zikadhaminiwa,
Za msingi zilizokuwa.

306.
Kisha kasma kupewa,
Elimu kutofifia,
Watu wazima raia,
Wakawa wanajisomea.

307.
Jioni wataingia,
Kusoma wapate jua,
Aidha kuandika pia,
Ya msingi kuyajua.

308.
Kama vyuo vitakuwa,
Maarifa kufunziwa,
Yatayoamuliwa,
Na wao wenyewe raia.

309.
Na wao wenyewe raia,
Eneo wanalokaa,
Wakafunzwa kujifaa,
Umoja na kujitegemea.

310.
Maradhi yanakimbia,
Ila mapya yaingia,
Na kasi yaliyokuwa,
Na kuongeza tanzia.

311.
Mikakati yatakiwa,
Hasa tiba kuvumbua,
Gharama kutokupaa,
Huduma watu kukosa.



312.
Wengi wanazihofia,
Hospitali Tanzania,
Waganga waogopewa,
Sio tena kudekewa.

313.
Nashauri Tanzania,
Kazi hizi kwangalia,
Daktari juu kuwa,
Ujira wanaopewa.

314.
Na manesi nao pia,
Njaa kutowavamia,
Ikawa rushwa wapokea,
Ndio watoe huduma.

315.
Wao wakidhulumiwa,
Na sisi tutaonewa,
Vipi wasiotufaa,
Ndio zaidi walipwa ?

316.
Kuanzia sasa yafaa,
Watumishi kupatiwa,
Ajira kwa kuzingatia,
Elimu wlaiyofikia.

317.
Hata waziri akiwa,
Vyetiwe kuviangalia,
Na kisha kudadavua,
Majukumu ya kufaa.

318.
Uzito kuongezewa,
Kama zaidi kapewa,
Ila hatutarajia,
Viongozi juu kuwa.

319.
Juu wanaotakiwa,
Mishahara kuchukua,
Ni tabibu Tanzania,
Na wanaotuokoa.

320.
Utamu pakufikia,
Wajuzi juu wakiwa,
Kazi waliobobea,
Wazuao ufumbuzi.



321.
Sera za watu kupewa,
Naona twapendelea,
Jasho pasina kutoa,
Swahiba wanyanyukia.

322.
Magwiji wanatakiwa,
Kazi zao kusomea,
Na kisha wakazijua,
Juu ndio kufikia.

323.
Wanasiasa wazua,
Wao wakajichotea,
Hali ukiangalia,
Kipato watukatia.

324.
Juu wanaotakiwa,
Njia wanazogundua,
Hazina ikawa yajaa,
Wala sio kupungua.

325.
Utamu wa kusifiwa,
Vyeo hivi kutungua,
Chini wakajishukia,
Majina yakabakia.

326.
Shule waliokimbia,
Kipato kikarejewa,
Na waliojinuia,
Haki yao kupatiwa.

327.
Elimu inatakiwa,
Kuwa ndiyo yetu taa,
Wengi inavyofikia,
Likawa lazawadiwa.

328.
Hapo tukishaifkia,
Na vihiyo kuishia,
Nchi itajiumua,
Mbele ikatangulia.

329.
Ila wanaotumia,
Za kwao za kuzaliwa,
Mambo wakatufanzia,
Wafaa kufikiriwa.

330.
Juu wakitunyanyua,
Na shule hawakujua,
Bado hao maridhia,
Wapaswa kuzawadiwa.

331.
Elimu fanifu kuwa,
Matatizo kuondoa,
Kila mwenye hiyo dawa,
Yafaa kumpa hidaya.

332.
Na elimu walopewa,
Wakashindwa itumia,
Wakawa watuibia,
Yafaa kuwaumbua.

333.
Kila mmoja akajua,
Ienzicho Tanzania,
Ni utumishi kutoa,
Si sura na kushangilia.

334.
Shule zetu Tanzania,
Mizani inatakiwa,
Tathmini kufanzia,
Viwango vyake kujua.

335.
Kuna hadhi kuwekewa,
Daraja tukalijua,
Za umma na za raia,
Uwiano kukisia.

336.
Hali zikahakikiwa,
Inavyokuwa dunia,
Wadau wakiridhia,
Yao yakakubaliwa.

337.
Ada tunapoanzia,
Kiasi tukakijua,
Thamani kudadavua,
Kila mtu akajua.

338.
Elimu kutoachiwa,
Kama vile duka kuwa,
Ila huduma ikawa,
Tunayoitegemea.


339.
Chakula kufikiria,
Lishe bora ilokuwa,
Menu wakazipatiwa,
Vyuo, shule kutumia.

340.
Kiwango juu kikawa,
Chini kutoshushiwa,
Hali ikawavutia,
Wageni kuja kusoma.

341.
Viwanja vinatakiwa,
Vya michezo kujengewa,
Kimataifa vikawa,
Ikatujua dunia.

342.
Somo la kujitegemea,
Bado nalipigania,
Shuleni kwenda tolwea,
Malezi kusaidia.

343.
Walimu tunatakiwa,
Idadi wanayotakiwa,
kwa darasa kutopungua,
Na kwa shule kuwajua.

344.
Mazoezi yatakiwa,
Watoto kujifanyia,
Homuweki wakapewa,
Pasina ya kukosea.

345.
Udhibiti watakiwa,
Ubora kuangalia,
Na mitaala kunyoa,
Aali kikabakia.

346.
Yafaa kulingania,
Binafsi na jumuiya,
Watu wakatambua,
Kweli linalotokea.

347.
Binafsi tukitumia,
Si tajiri tumekuwa,
Kiwango waangalia,
Nafasi kushindania.



348.
Ya juu inapokuwa,
Wana kutowabagua,
Umma na binafsia,
Usawa wote kupewa.

349.
Sasa rushwa Tanzania,
Adui mkubwa kawa,
Vyama zinaipokea,
Achia wao raia.

350.
Kanuni zinatakiwa,
Adui kumshambulia,
Maana wanaomujua,
Wasema hawajamjua.

351.
Ufafanuzi walia,
Lazima wapate pewa,
Mimi sijawalewa,
Ila naona nazaa.

352.
Rushwa ninavyoijua,
Ni kitu chochote kutoa,
Utakacho ukapewa,
Hata haramu ikiwa.

353.
Dola ikishafulia,
Mangimeza kuitwaa,
Udhibiti ukavia,
Basi hapo hustawi.

354.
Polisi wa Tanzania,
Kwalo hili wasifiwa,
Trafiki wamejaa,
Vipi zavunjwa sheria?

355.
Nyama wanaonunua,
Mchana ukiingia,
Ukienda ulizia,
Ni nani utaambiwa.

356.
Daladala kwenye njia,
Bodaboda nazo pia,
Bajaji ndio balaa,
Wamiliki wamekuwa!


357.
Vipi zitaheshimiwa,
Za kwetu nchini sheria,
Hali wao wajijua,
Wameshajitapikia ?

358.
Ila wanaojijua,
Vishawishi huvitoa,
Na mianya kubomoa,
Nchi salama ikawa.

359.
Magari wakinunua,
Mafuta ni ya kununua,
Mtu gari hujaliwa,
Ila mafuta hanayo.

360.
Mifukoni yatokea,
Hifadhi isiyokuwa,
Hapo hukugeukia,
Mstaafu kuibiwa.

361.
Ufisadi nao pia,
Kwetu sasa adawa,
Nje wanatoroshea,
Uswizi kujifichia.

362.
Ukabila Tanzania,
Naona waja mpya,
Wa kichama ulokuwa,
Kimoja wapendelea.

363.
Chamani usipokuwa,
Ugumu mamboyo huwa,
Viwanja kwa kuanzia,
Na biashara kwingia.

364.
Wao wajipendelea,
Wengine wanaonewa,
Haki sasa walilia,
Nchi yetu kutawala.

365.
Haki zikinunuliwa,
Uadui tunazua,
Polisi kuangaliwa,
Kwenye hili wabobea.



366.
Mahakimu nao pia,
Na mtu wakitumiwa,
Haki kweli itakuwa,
Hapa kwetu Tanzania?

367.
Kuna adui tamaa,
Na uchu ulioingia,
Watu wajitangazia,
kama tiketi kupewa.

368.
Wengine wakanunua,
Matope kuwapakaa,
Wao bora kujitia,
Ilhali twawajua!

369.
Matajiri Tanzania,
Adui waweza kuwa,
Wakianza kuvamia,
Ya imani kubomoa.

370.
Kuna miko yatakiwa,
Kwenye vitu kununua,
Wakfu inapokuwa,
Mara mbili fikiria.

371.
Mizimu inasikia,
Kwa wale wasiojua,
Huja hapa kurejea,
Ya kwao kuangalia.

372.
Wakikuta chaibiwa,
Hasira huwaingia,
Ukabaki kujutia,
Ya nini ulizaliwa.

373.
Nyumba kutokujengewa,
Naona tunachukiwa,
Hali wengine wapewa,
Hali chini wazikosa.

374.
Au shere twachezewa,
Na juu waliokuwa,
Ili yao kuja kuwa,
Budi viotani twishi?

375.
Katiba ingeamua,
Haki kuitangazia,
Nyumba kwa kila familia,
Lazima tukajengewa.

376.
Cuba walijifanzia,
Mengine kushughulikia,
Tatizo wakaliondoa,
Maendeleo kuzua.

377.
Hapa kwetu Tanzania,
Mkakati watakiwa,
Ikapeana mikoa.
Ili nyumba kujengeka.

378.
Viwanda watavizua,
Na ajira kuzitoa,
Yataka kujipangia,
Wito moyoni ukawa.

379.
Pawe katika mkoa,
Kuna wilaya kadhaa,
Kazi wanajipangia,
Kilimo kutumikia.

380.
Mkoa mmoja ukawa,
Kwa hali unajigawa,
Nafaka wakazizaa
Na ya biashara pia.

381.
Baadhi wawe wavua,
Kwa mabwawa kuyazua,
Samaki wakajilimia,
Na uchumi ukakua.

382.
Mboga mboga zatakiwa,
Ikachaguliwa wilaya,
Kujakulisha mkoa,
Na nje kujiuzia.

383.
Ufugaji kwa maziwa,
Na nyama unatakiwa,
Proteni zatuishia,
Na akili kupungua!


384.
Kweli ukitembelea,
Vijiji vya Tanzania,
Vingine utagundua,
Wahitaji kidogo tu.

385.
Mkakati hivi kuwa,
Kama biashara yawa,
Haraka tukajifanyia,
Hamsini yasochukua.

386.
Wanaweza kujinoa,
Ufakiri kuutoa,
Daraja wakanyanyua,
Kama watu nao kuwa.

387.
Ila juu walokuwa,
Watakiwa jionea,
Visa wakavisikia,
Na tiba kuichangia.

388.
SACCOS zikazaliwa,
Za ujenzi Tanzania,
Huko ikaongezewa,
Na simu wasiotoa.

389.
Watu watazichangia,
Ili kufika hatua,
Mtu akajikopea,
Deni la nyumba kulipa.

390.
Itang'aa Tanzania,
Hata vijijini pia,
Watu tukawanyanyua,
Ngazi mpya kufikia.

391.
Uhuru twajivunia,
Wa bendera ulokuwa,
Misingi imetwekea,
Tunaweza kutumia.

392.
La muhimu kutanua,
Uhuru ukaenea,
Nafsi zikaridhiwa,
Na makundi kujaliwa.



393.
Tunayoyazungumzia,
Tukaona yanafaa,
Sababu sijaijua,
Kwanini kutotelezwa ?

394.
Mfano naulizia,
Tume huru ilokuwa,
kwanini tunakawia,
Na ukweli twaujua?

395.
Mipaka hadhi kutia,
Kama viwanja vikawa,
Ndege tunakopandia,
Na sisi kuheshimiwa.

396.
Mutukula na Namanga,
Tunduma ni kuengaenga,
Hadhi mbele ikasonga,
Raia kujivunia.

397.
Mipakani na Rwanda,
Burundi nako kuranda,
Watu wanapokwenda,
Udhia uwe muhali.

398.
Msumbiji na Zambia,
Malawi na huko pia,
Asafiri Mtanzania,
Hali salama akiwa.

399.
Hakuna kuendelea,
Bila kuwa na ubia,
Nasi wanaotufaa,
Jirani watuzungukao.

400.
Mipaka bora ikiwa,
Biashara kuinua,
Na uchumi hupanua,
Soko kubwa kufikia.

No comments:

Post a Comment