MTANZANIA una haki ya wewe kuwa na mwakilishi katika chombo kitakachozungumzia na kisha kusaidia kazi ya kuandika katiba mpya. Katika wakati huu, wewe mwananchi, raia wa Tanzania unapanda cheo na kuwa ndiye mwajiri wa rais,makamu wa rais, mawaziri, wabunge na watumishi wote wa serikali. Kazi yangu katika mchakato huu ni kuwaambia viongozi hao kwamba: 'tunawataka mtutawale hivi na uwezo na sifa zenu ziwe hivi. Kinyume cha hivyo tutawafuta kazi..' endelea kurasa inayofuatia:
Sunday, February 17, 2013
UTENZI WA KAITBA MPYA TANZANIA 401-600
UKMT 401-600
401.
Tuwe ni wa kuanzia,
Wala si wa kungojea,
Kama taa Tanzania,
Tuangaze yao njia.
402.
Tanzania mshumaa,
Jirani waangalia,
Kitu tukikianzia,
Fedha ndani tutatia.
403.
Bandari kuiokoa,
Vifisadi kuvitoa,
Aibu wanaotia,
Jirani wakatuchukia.
404.
Bandari salama kuwa,
Mfano wa kutambuliwa,
Nchi ikajivunia,
Afrika kufurahia.
405.
Yafaa kufatilia,
Kila siku, kila saa,
Maana tunapajua,
Huko wankotwibia.
406.
Sahani tukiandaa,
Watumishi kuingia,
Wote tukafurahia,
Ya ukweli kuyajua.
407.
Watumishi wasifiwa,
Na wema waliokuwa,
Ila mabosi udhia,
Njaa imewazidia.
408.
Ukweli watatoboa,
Chini wanaoumia,
Hadi nguo kuzivua,
Wakubwa uchi wakawa.
409.
Bandari ikishang'aa,
Itawaza Tanzania,
Mabilioni kutwaa,
Tena yasijepotea.
410.
Mikoa inatakiwa,
Uchumi kuangalia,
Uhuru ikipatiwa,
Ushindani watazua.
411.
Ushindani wakizua,
Mikoa haitafifia,
Yao watapigania,
Wajezuka kidedea.
412.
Nishani tukizitoa,
Ziwe zinashindaniwa,
kati ya yetu mikoa,
Nguvu itaziumua.
413.
Na ukuu wa mkoa,
Wakati unaishilia,
Sasa anatakiwa,
Waziri Mkuu Mkoa.
414.
Naye akasaidiwa,
Na bunge la wake mkoa,
Ujerumani wajua,
Walioitembelea!
418.
Mawaziri huchagua,
Mkoa kujijengea,
Uchumi pia jamaa,
Wao wakaangalia.
419.
Serikali nchi kuwa,
Ulinzi yaangalia,
Na usalama kulea,
Kitaifa inafaa.
420.
Serikali bora kuwa,
Fedha inasimamia,
Kasma yake kutwaa,
Na wengine kuachiwa.
421.
Uchumi huangaliwa,
Mkazo ukatiliwa,
Pale nguvu zilokuwa,
Haraka za kuendelea.
422.
Mfano niliutoa,
Wa ujenzi Tanzania,
Watu tukawapatia,
Haraka nyumba kukaa.
423.
Itakuwepo mikoa,
Matofali yafyatua,
Na wengine kuuzia,
Kipato chao kikawa.
424.
Itakuwepo mikoa,
Samani inaandaa,
Milango kuiandaa,
Dirisha na kabati pia.
425.
Wengine wakanunua,
Mbao na kuzitumia,
Samani kujichongea,
Wenzao kuwauzia.
426.
Itakuwepo mikoa,
Vigae kujichomea,
Bilioni kufyatua,
Ujenzi ukaenea.
427.
Itakuwepo mikoa
Tailzi itachangia,
Uchumi tena kwa mia,
Ikawa wahesabiwa.
428.
Wataagizwa Songea,
Mafundi wa kujengea,
Ndanda na huko wajua,
Kwa wingi wakaajiriwa.
429.
Ikawa inachanua,
Hii yetu Tanzania,
Kwa umoja kujengewa,
Maskani tukakaa.
430.
Hali wanaajirwa,
kwa wingi waliokuwa,
Vijana wakitembea,
Pasi kazi kuijua.
431.
Uchumi ni kuamua,
Wapi tunaelekea,
Na siasa za ujamaa,
Kama bado zinafaa.
432.
Awali niliwambia,
Debe mie napigia,
Ubepari-ujamaa,
Siasa yetu ikawa.
433.
Na yake kubwa nadharia,
Ni uchumi huru kuwa,
Watu wakaruhusiwa,
Juu sana kujipandia.
434.
Juu sana kujipandia,
Pasiwe na kuzuiwa,
Ila kanuni kuzua,
Fukara kutoumia.
435.
Neti tutaiandaa,
Ya kiuchumi ilokuwa,
Kwa kodi kuzitumia,
Na maduhuli ya ubia.
436.
Navyo tuanvyojivunia,
Kwa dhahabu kuchimbua,
Na mali asili kuzaa,
Mfuko wa kusaidia.
437.
Elimu bure ikawa,
Usawa inayojua,
Hadi chuo kuingia,
Makato wakaanzia.
438.
Afya itaangaliwa,
Maskini kutodaiwa,
Wazazi kujifungua,
pasina kuwa udhia.
439.
Benki kuu kuandaa,
Kusaidia wazawa,
Ujasirmali kufaa,
Watu wakajinyanyua.
440.
Mitaji kupalilia,
Ya jamii ilokuwa,
Hapo tukaanzilia,
Kisha hatima kukua.
441.
Rasilimali radhia,
Watu wote kuwafaa,
Hao wanaoidokoa,
Budi kushughulikiwa.
442.
Yatakiwa Tanzania,
Mkakati nao kuwa,
Kukuza teknolojia,
Ili tusije chelewa.
443.
Rwanda tumeiachia,
Sasa yatutangulia,
Aibu ninajisikia,
Kila ninapojionea.
444.
Ilikuwa Tanzania,
Ya kwanza ingelikuwa,
Sera tuliiandaa,
Na kanuni kuanzia.
445.
Wanasiasa balaa,
Gurudumu wazuia,
Badala kuendelea,
Nyuma tunajirudia.
446.
Mamlaka yatakiwa,
Hili kulisimamia,
Huru itakayokuwa,
Si kama idara kuwa.
447.
Wajuzi wanatakiwa,
Mbele wanaoangalia,
Mambo wakayatambua,
Ielekeyako dunia.
448.
Vijitu tukitumia,
Vidudu tutabakia,
Nami sintoshangaa,
Zaidi tukilegea.
449.
Sera kubwa yatakiwa,
Vitu vingi kuvumbua,
Miaka iliyotimia,
Hamsini twaijua.
450.
Hamsini twaijua,
Toka uhuru kupewa,
Bado tuantegemea,
Vya nje kuvinunua?
451.
Aibu imetuishia,
Na haya twajiuzia,
Wataalamu wavia,
Kwa siasa kusambaa!
452.
Mipaka itanadiwa,
Utaalamu kupea,
Yake ukaangalia,
Na kilele kufikia.
453.
Siasa tukiachia,
Hazijengi, zabomoa,
Na taifa likavia,
Hadi tukalichukia.
454.
Trekta tungeanzia,
Katiba kulitambua,
La taifa latakiwa,
Humu humu likaundwa.
455.
Pampu zinatakiwa,
Viwanda vyetu kuzaa,
Fahari gani ikawa,
Paisna kujitegemea?
456.
Halafu ikafatia,
Nyumbu kuifufua,
Lori litakalokuwa,
Kama Yue Jin la China.
457.
Mikoa huru ikiwa,
Yatakiwa kuamua,
Uchumi kuwa ubia,
Wakazi ikanyanyua.
458.
Kuna mengi yanafaa,
Kwa pamoja kwandaliwa,
Kilimo, viwanda pia,
Uchumi kuustua.
459.
Aidha maji kujua,
Na wote yanatakiwa,
Ubia unapokuwa,
Shughuli huangaliwa.
460.
Umeme rahisi kuwa,
Ikizalisha mikoa,
Iweze kujitoshea,
Na mwingine kujiuzia.
461.
Viwanja vinatakiwa,
Kujengwa na kufufuliwa,
Hadhi ikajipandia,
Na wana kusaidia.
462.
Vyuo vikuu vyakua,
Kila mkoa vyatakiwa,
Ubia wakiingia,
Ugumu hawatojua.
463.
Na mikakati kutiwa,
Viongozi kuchagua,
Sio wa kuzawadiwa,
Ambao ni marejea.
464.
Masoko yakibuniwa,
Vitakiwavyo kutoa,
Hakuna kitachopungua,
Juu kupaa mikoa.
465.
Shule nzuri wakizua,
Nje watakujajisomea,
Ada wanayolipia,
Za kigeni kuingia.
466.
Hospitali kuzizua,
Wagonjwa wakatibiwa,
Nje waweza tokea,
Ikawa ni manufaa.
467.
Katiba inatakiwa,
Muongozo kuutoa,
Uchafu kuukata,
Tusiwe twavumilia.
468.
Miji yetu bora kuwa,
Na vijiji navyo pia,
Wazungu wakashangaa,
Wakadhania Ulaya.
469.
Ndani yetu limekaa,
Sio la kutegemea,
Siasa zinatakiwa,
Pembeni kuziambaa.
470.
Kubwa linalotakiwa,
Mitambo ya kurejelea,
Taka zilizoingia,
Zikageuzwa bidhaa.
471.
Seychelles naambiwa,
Mashine wajiundia,
Huko ningelitembea,
Badala kuranda Ulaya.
472.
Takataka tukijua,
Bidhaa zaweza kuwa,
Nyingine kurejelewa,
Vifaa tukatumia.
473.
Karatasi tukatoa,
Na plastiki nazo pia,
Na chupa kumiminiwa,
Kama mpya kurejea.
474.
Takataka ni mbolea,
Tena sumu isokuwa,
Sisi tunazichezea,
Na miji kuichafua.
475.
Mifereji tungejua,
Bayogesi ingetoa,
Chini kwa chini ikawa,
Mavuno twajivunia.
476.
Maji ya chumvi pia,
Baridi yaweza kuwa,
Nyumbani yakatumiwa,
Na shambani kumwagiwa.
477.
Katika ikichochea,
Haya yatagunduliwa,
Nchi ikajititimua,
Daraja bora ikawa.
478.
Kwa hayo tutatokea,
Mengine kuingilia,
Na watoto kuwaahcia,
Mengine wakagundua.
479.
Uhuru tukipanua,
Mengi tutajiundia,
Kuna wanaozaliwa,
Redio wajua tengeza!
480.
Ila wanadhulumiwa,
Na vifungo kutishiwa,
Hawa tungewaachia,
Mitambo watagundua.
481.
Kuna wanaopokea,
Cha wazungu nasikia,
Watoto kuwazuia,
Vya kwetu kuvivumbua.
482.
Katiba kuangalia,
Vipi twaweza kulea,
Wana wanaogundua,
Hadi tukavitumia.
483.
Wawe wasiouzuiwa,
Kisha ari kung'olewa,
Kama viza kutamiwa,
Kitu kisichoanguliwa ?
484.
Pasina wa kutamiwa,
Wanunuzi twabakia,
Katika hii hatua,
Vibovu watauuzia.
485.
Vyetu tukijiundia,
Vya ovyo havitakuwa,
Pia tutavielewa,
Na kurekebisha kwake.
486.
Gharama hatutaingia,
Nje kwanda agizia,
Maana ndani vyazaliwa,
Haja zetu kuzikidhi.
487.
Utamdauni wavia,
Baraza lasahauliwa,
Kichekesho kinakuwa,
Wazungu kuwategemea.
488.
Wazungu kuwategemea,
Utamaduni kulea,
Aibu imetupaa,
Na uso kuubinua?
489.
Utamaduni radhia,
Wazawa huangalia,
Na kinachotamaniwa,
Fungu pembeni kupewa.
490.
Ofisi zao kinyaa,
Kila idara na jaa,
Nani wa kuangalia,
Wote 'bize' wanakuwa?
491.
Na lugha tukianzia,
Ushauri nautoa,
katiba kuja amua,
Mamlaka yaundiwa.
492.
Mamlaka yaundiwa,
Huru itakayokuwa,
Kizibao kutovaa,
Wizara kutumikia.
493.
Mamlaka ya Kiswahili,
Itakuwa ni kamili,
Tena ni chombo halali,
Lugha kuiangalia.
494.
Vyanzo itachanganua,
Miradi kujianzishia,
Kipato kikaingia,
Yenyewe ikaamua.
495.
Ziengwe rasilimali,
Kutufaa bilkuli,
Sasa kwa ilivyo hali,
Ufisadi umejaa.
496.
Juu walojikweza,
Wataka kuzimaliza,
Wawa kama waigiza,
Ila wanatuchuuza.
497.
Mikataba waridhia,
Kama vile ya kijuha,
Au wananunuliwa,
Psina sisi kujua.
498.
Sasa kinachotakiwa,
Tamko leltu kutoa,
Rasilimali ni dia,
Twazimiliki raia.
499.
Pale kwetu tukivua,
Hiyo ni yetu ngekewa,
Mola katubarikia,
Japo hatukulijua.
500.
Iwepo asilimia,
Daima ya kuachiwa,
Kisha ndiyo kugaiwa,
Kitaifa Tanzania.
501.
Thamani kuichungua,
Iwe ni yetu tabia,
Na huo mtaji ukawa,
Kwa wazawa walokuwa.
502.
Waweza kujiuzia,
Au hisa kuridhia,
Umiliki wakajua,
Hali wanajinyanyua.
503.
Kijiji kikiamua,
Ubia kitawania,
Yao wakajifanyia,
Kisha wakajichomoa.
504.
Wakubwa wanayofanza,
Imani wanaikwaza,
Twaona wanajitunza,
Pekee wakajaliwa.
505.
Wao wakishapatiwa,
Sisi husahauliwa,
Mshirika wao kuwa,
Mwekezaji Tanzania.
506.
Tunaona wanapwaya,
Urahisi wanajitia,
Kidogo wanachopewa,
Sisi hatwezi kizaa ?
507.
Wanatakiwa kukua,
Njaa kuacha ugua,
Ili wapate tambua,
Tukijipanga twaweza.
508.
Wote tukijigawia,
Wala hakitapungua,
Na kinachowazuzua,
Kaburi lawaangia.
509.
Yatayokujakutokea,
Mazuri hayatakuwa,
Salama hapatakuwa,
Ila maisha kuvia.
510.
Vipaji vya tasnia,
Katiba inatakiwa,
Muongozo kuutoa,
Kwa haki vikalelewa.
511.
Sasa yanayotokea,
Mmoja mmoja kuwa,
Mwenyewe akiamua,
Nani kumsaidia.
512.
Mifumo kuandaliwa,
Vyote vikakaguliwa,
Na zikawepo sheria,
Hili kuliangalia.
513.
Watoto wa Tanzania,
Haki sawa watakiwa,
Pasiwe kupendelea,
Na wengine kuonewa.
514.
Vijana wa Tanzania,
Fursa sawa kupewa,
Sio kwa vitendo na nia,
Ila kwa kazi kufanziwa.
515.
Wazee wanatakiwa,
Baraza wakaundiwa,
Wala sio kutumiwa,
Kama vile kitambaa.
516.
Kama vile kitambaa,
Mikono kujifutia,
Ila wakatunukiwa,
Nchi kuizungumzia.
517.
Nchi kuizungmzia,
Pasina kuegemea,
Na kama ni kuamua,
Haki ikatangulia.
518.
Yao pia kwangalia,
Nafuu kujipatia,
Sasa wasahauiwa,
kila mtu anajua.
519.
Twaweza waangalia,
Mchabgo bora kutoa,
Nchi ikatengamaa,
Imara ipate kuwa.
520.
Wazee wamejaliwa,
Umri walioukaa,
Maisha wanayajua,
Na vituko kung'amua.
521.
Wasipokuwa na njaa,
Huingia ushujaa,
Udhia wakakataa,
Halali kupigania.
522.
Ndivyo inavyotakiwa,
Mchango bora kutoa,
Nchi ikaendelea,
Kwa aali nadharia.
523.
Kinamama watumiwa,
Na uchama kuwagawa,
Sasa fedha wagagawiwa,
Wengine kuwazomea.
524.
Vigelegele watia,
Ili wongo kufukia,
Kisha wakashangilia,
Ya haki yasiyokuwa.
525.
Baraza linatakiwa,
Zama lililoogopewa,
BAWATA kulifufua,
Umoja ikawania.
526.
Nchi hii yenye njaa,
Ujanja inatumia,
Wote wanaoishiwa,
Rahisi kununuliwa.
527.
Katiba inatakiwa,
Jambo hili kuzuia,
Kama ni kwendelea,
Juhudi zao kutia.
528.
Mambo ya
kunyanyuliwa,
Mengine yana udhia,
Mzungu twamnyania,
Yatakuja tuumbua.
529.
Katiba ingelifaa,
Majina kuyazuia,
Mwenyezi yanayomfaa,
Binadamu kutumia.
530.
Viongozi wakapewa,
Vichwani yakaingia,
Sumu kuwageukia,
Wakaiva kwa ubaya.
531.
Utukufu kuanzia,
Hilo kutoruhusiwa,
Qudusi aliyekuwa,
Mmoja mwingine hakuna.
532.
Mtakatifu hadaa,
Kiumbe hawezi kuwa,
Hili kutolitumia,
LIkakoleza balaa.
533.
Yatosha waheshimiwa,
Makengeza kutumia,
Hao ndio wahishimiwa,
Daima wanaoishiwa.
534.
Mwenyezi si wa kuishiwa,
Wala hawezi pungukiwa,
Sifa hiyo kajaliwa,
Binadamu alopewa.
535.
Mabunge tukijaliwa,
Aina mbili yakawa,
La wanaochaguliwa,
Na wanaoteuliwa.
536.
Maji kucha kutia,
Bunge la kuchaguliwa,
katiba ingekazia,
Vinginevyo kutokuwa.
537.
Watoto wanaumia,
Na sisi twaangalia,
Ukimwi kwa kuanzia,
Wazazi wawachukua.
538.
Hakuna lililokuwa,
Tayari tumelivumbua,
Kama chombo hicho
kuwa,
Hawa kuwaangalia.
539.
Inadorora jamii,
Kwa wakubwa kutotii,
Kiapo walichotanabahi,
Vyeoni wakiingia.
540.
Watu hawatumikii,
Kutumikiwa wadai,
Wakauzira uhai,
Na watu kuwachukia.
541.
Uongozi watakiwa,
Kiutu ulokomaa,
Usongoja kusifiwa,
Ila unaojitolea.
542.
Kinamama walofiwa,
Na waume nao pia,
Mayatima Tanzania,
Uyatima wakomaa.
543.
Nani wa kuwaangalia,
Ila wa kuwahurumia,
Katiba inatakiwa,
Hili likatatuliwa.
544.
Tunazo rasilimali,
Zinatosha kulhali,
Kushindwa uanzali,
Au utu watuishia.
545.
Hili pia laendana,
Nao mitaani wana,
Walikuwa wachache
jana,
Hivi leo ni mamia.
546.
Tutakuja pata laana,
Hili tusipolisana,
Yetu tukaharibiana,
Kwa hawa kuwaambaa.
547.
Watakuja
changanyikana,
Wakashidnwa elewana,
Wakaanza
kupambana,
Dhiki zikawanukia.
548.
Mifumo tumeishiwa,
Wala wengi hawajawa,
Ari tungelijaliwa,
Haya yasingetokea.
549.
Vijana twawaachia,
Paka tukawatishia,
Hofu zikiwaishia,
Tuna letu nawambia.
550.
Sasa kinachotakiwa,
Ni miundo kuzindua,
Na mifumo kufumua,
Upya tukajishonea.
551.
Hatuwezi tukalia,
Ajira zinapotea,
Na matatizo twajua,
Kedekede yamejaa.
556.
Mianya budi kutoa,
Wakubwa kupendelea,
Makwao kulikokuwa,
Jamhuri yote sawa.
557.
Fursa kutozuia,
Upinzani kuchanua,
Na wnakojishindia,
Nako kukaendelea.
558.
Matatizo Tanzania,
Fursa yaweza kuwa,
Vijana wakielewa,
Ajira kwao ikawa.
559.
Nyumba hatujajaliwa,
Na kiasi zapugnua,
Vijijini kunapwaya,
Si nyumba viota huwa.
560.
Miradi tukianzia,
Matofali kufyatua,
Benki kuu kwangalia,
Vipi itasaidia.
561.
Mikoa kuchaguliwa,
Watakaoyafyatua,
Na wengine wakawa,
Mengine wajifanyia.
562.
Vigae vinatakiwa,
Mkoa kazi kupewa,
Vijana ikatumia,
Wakajikimu kwa hili.
563.
Milango inatakiwa,
Na mbao waliokuwa,
Wataweza jiundia,
Au mbadala kuzua.
564.
Tailzi zinatakiwa,
Sakafuni zikatiwa,
Kama tukiazimia,
Vijana wataandaa.
565.
Dari watatengeneza,
Kwenye nyumba
kueneza,
Vijumba vikapendeza,
Na hadhi tukajipatia.
566.
Kilimo tukiamua,
Kitaajiri mamia,
Mtadi tukijitoa,
Kimasomaso ikawa.
567.
Msingi wakipatiwa,
Na chakula kugawia,
Wapo wataoridhia,
Kwenda kujitegemea.
568.
Na uvuvi nako pia,
Aidha na kujifugia,
Na viwanda kuvizua,
Vya msingi kuzalisha.
569.
Vijijini nawambia,
Kwingine kwanistua,
Milioni wakipewa,
Wanaweza kujitoa.
570.
Wanaweza kujitoa,
Uongozi wakipewa,
Haya unayoyajua,
Njia ukawaonyesha.
571.
Taasisi zimezuka,
Huko hazijawahi fika,
Elfu kumi zinataka,
Zikaweza kukomboa.
572.
Benki kuu ikitaka,
Mayai inayoweka,
Ikatamia hakika,
Nchi juu itapaa.
573.
Pesa kidogo ni dawa,
Matatizo kuondoa,
Masikini walokuwa,
Utajiri kunukia.
574.
Labda upo mwongozo,
Ulifanyalo mzozo,
Waogopa wenye nazo,
Umaskini ukiisha?
575.
Minong'ono yajaa,
Mtaji uliozuliwa,
Ni umasikini kulea,
Kutawala Tanzania.
576.
Makabila Tanzania,
Urithi tulojaliwa,
Uhaini kuyaua,
Kwa lolote lilokuwa.
577.
Umoja tumejaliwa,
Twajivuna Tanzania,
Kitakachouondoa,
Ufisadi si kabila.
578.
Matabaka yataua,
Si ukabila wa lugha,
Umoja tuliouzua,
Mbali wakajitupia.
579.
Rushwa itauondoa,
Si makabila Tanzania,
Kwa jinsi inavyoenea,
Na watu kuivumilia.
580.
Makabila kuenziwa,
Iwe ni yetu tabia,
Makumbusho yakapewa,
Kuhifadhi historia.
581.
Na kwayo teknolojia,
Lugha zikahifadhiwa,
Nani anayeyajua,
Mbele yatatusadiia?
582.
Kawaida ni sheria,
Kwa watu wasiojua,
Udini ukitumiwa,
Hili kuondoa baa!
583.
Wapo wanaojizuzua,
Kawaida kuiua,
Budi kushughulikiwa,
Ndiyo haki ilokuwa.
584.
Mapya tukizuia,
Kwa vitisho kutumia,
Raia watachukia,
Na kisasi kukitia.
585.
Watazidi kuroroma,
Na kuzizusha nakama.
Pakawepo uhasama,
Wa kijinga Tanzania.
586.
Mfano hili la kuchinja,
Wajua kina Masanja,
Dini moja walichinja,
Na wote tukaridhia.
587.
Ugumu halijakuwa,
Kuliko vita kuzua,
Serikali kuamua,
Pagani kuruhusiwa?
588.
Wagomvi wanaokua,
Vidogo huingilia,
Ukubwa wakautia,
Wapate kutambulika.
89.
Mabucha tukayatenga,
Yao yakatabandanga,
Na halali kuyakinga,
Yasije kuchafuliwa.
590.
Kuna wana Tanzania,
Wembe sasa walilia,
Kwa moja kuligundua,
Wadhani yote wajua.
591.
Kazi tukijipangia,
Na ufanisi zikawa,
Ufanifu nao pia,
Budi kuuangalia.
592.
Idadi ikizidia,
Kazi tunaichafua,
Kiasi inatakiwa,
Kutosha ni maridhia.
593.
Kisha wanaozipewa,
Kazi zao wakajua,
Sio kutunukiwa,
Madudu yatatujaa.
594.
Wajuzi waliokuwa,
Kazi zao kuachiwa,
Siasa zikiingilia,
Taifa hukorofisha.
595.
Ujira kuangalia,
Riziki ikatimia,
Kila inapopungua,
Uovu mpya huzua.
596.
Masoko yanatakiwa,
Kwa wakuu kuyajua,
Wasiishie tembea,
Pasina cha kujiuzia.
597.
Balozi zingetakiwa,
Rasimu kuiandaa,
Kila nchi tukajua,
Nini cha kujiuzia.
598.
Nini cha kujiuzia,
Na rahisi kununua,
Wasiishi na kukaa,
kama vile matajiri.
599.
Hujisahau balozi,
Nchi wakawa hawawazi,
Wakaishia usingizi,
Na tija usiokuwa.
600.
Kufunzwa wanatakiwa,
Ujasiramali tabia,
Kazini kuutumia,
Wakistaafu pia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment