KAMA sehemu muhimu ya Ulinzi na Usalama wa nchi ni lazima kuwe na
wawakilishi wa uhakika na watakaochangia juu ya fikra na mtazamo mpya kuwa
nini iwe ni nafasi ya majeshi yetu ya ulinzi na usalama baada-Katiba mpya.
Kuna maswali kadhaa yakujiuliza:
i. Turuhusu kama nchi nyingine za kishenzi zinavyofanya kuwasakazia
raia polisi na jeshi. Na kisha kuwatia ulemavu, kuwajeruhi na hata kuwaua na
hivyo kusababisha wake kukosa waume na watoto kukosa baba na mama. Kiasi
kwamba tunamfanya Mtanzania mmoja akubali kuelekeza mtutu wa bunduki na
kufyatua risasi dhidi ya baba yake, mama yake, mwanawe au mjukuu wake?
ii. Kwanini Mkuu wa Polisi asiteuliwe na kuwa mtii kwa Bunge tukufu la
nchi yetu baada-Katiba ?
iii. Kwanini majeshi yasiape kuwa watii na waaminifu kwa WANANCHI WA
TANZANIA na siyo rais tu. Na katika kuchagua wapi pa kuegemea sikuzote
wachague wananchi na sio viongozi walioko madarakani ?
iv. Tuzuie vipi rushwa ya kifedha, kicheo, kisiasa na nyinginezo katika
majeshi yetu ?
v. Kwa kuzingatia kujitoa mhanga kwa polisi na wanajeshi wetu ni
mshahara gani unaostahili kuwa kima cha chini kwa jeshi ili wasishawishike na
rushwa za aina zote?
vi. Je, polisi na jeshi tukiacha siasa za Uswahilini waishi katika jamii au
wawe na makambi maalum?
vii. Nni nafasi ya majeshi na polisi wetu katika kuhakikisha amani na
usalama kwa kuchangia amani na usalama wa nchi jirani?
viii. Nini kiwe kiwango cha chini cha elimu kwa askari polisi na wanajeshi
katika karne hii ya sayansi na teknolojia?
ix. Je, Polisi jamii kweli wanahitajika au huku ni kukoroga mambo
kutokana na kuishiwa kimawazo kwa viongozi wetu na kwamba katika nchi hii
pawe na specialization na sio kila 'jack and jill' aweze kuwa askari?
x. Je, wakati wa amani na salama nchini majeshi yetu kwanini yasiingie
katika shughuli za uzalishaji mali na kuisadia jamii kupata mahitaji yake ya msingi
haraka zaidi badala ya sisi kuishi kama vile Mtanzania wa leo ataishi milele?
xi. Nini kifanyike ili polisi, jeshi na wanausalama wetu wasitumiwe hata
kidogo na vyama vya siasa na wanasiasa wetu na kutuvuruga Watanzania na
nchi yetu ?
WATAKAOCHANGIA bila uchama, ukabila, ueneo, udini, ubinafsi na ushawishi wowote toka kundi lolote ndani au nje ya nchi watastahili kupewa tunzo ya juu kabisa ya Kitaifa.
NI haki na wajibu wenu pia kuwaamsha, kuwafundisha na kuwaelekeza wananchi wengine nini wanachopaswa kufanza ili mahitaji yao ya msingi, dhiki, mapungufu kwao, kasoro zilizopo kwenye maeneo na maisha yao, haki na maslahi yao yote yaweze kupatikana kwa kutumia katiba na sheria za nchi na sio vinginevyo.
Ni muhimu pia wananchi kuelewa kwamba serikali ni kitu kinachodumu milele mpaka mwisho wa dunia lakini vyama vya kisiasa ni taasisi za kupita, leo vinaweza kuwepo na kesho visiwepo na vikaja vyama vipya kabisa madarakani.
WATANZANIA tuna kila sababu ya kuikataa tabia inayojitokeza na kujijenga Afrika ya kuwatumia polisi na wanajeshi wetu kuwapiga, kuwatia ulemavu au hata kuwaua baba zao, mama zao, ndugu zao, kaka zao, dada zao, watoto wao, rafiki na jamaa zao. Na hili linataka demokrasia kamili, pana, refu na ya kina lakini wakati huo huo ikikataa usiri, uozo, uongo, ulaghai na kuwadanganya wananchi na rushwa, wizi na ufisadi unaolindwa na kuenziwa na chama cha kiasiasa ili kiendelee kubaki madarakani milele.
No comments:
Post a Comment