VIONGOZI wetu wa kisiasa wametuambia kunanukia gogoro la kidini nchini. Mnakubali wazee, masheikh, maaskofu, manabii (wa enzi hizi zisizosthaili kuwa na manabii) na wahashamu na watukufu wetu je, huu si muda muafaka wa kuweka kila kitu hadharani kuhusiana na mahusiano kati ya dini na waumini wake; ;dini na serikali; dini na dini nyingine; dini na vyama vya siasa; dini na mahakama; dini na vyombo vya habari; dini na wafadhili wa ndani na nje; dini na shule, vyuo, na vyuo vikuu vyake; dini
na zahanati au hospitali zao; dini na redio au televisheni zao; na mahusiano mengine yoyote ambayo yatakuwa na umuhimu katika kutusaidia kuwa na katiba itakayotuepusha na gogoro la kidini na yale yanayotokea katika nchi kama Rwanda, Burundi, Misri, Cote d'Ivoire, Nigeria na nyinginezo kama hizo.
KInachotakiwa hapa ni kwa viongozi wa dini kuketi katika dini zao na kisha pengine kupitia WRPC ambayo ni taasisi inayoziunganisha dini zote kuzungumzia kwa pamoja mapendekezo yao kwa mchakato huu wa katiba uende vipi? Mtajua wenyewe kama mtapendekeza pia Tume kufanya kazi hiyo na mchakato mzima kusimamiwa na rais na serikali yake au mchakato huu ufanyike kupitia Baraza au Mkutano wa Katiba Mpya 2011 kama wenzetu wa Kenya na Zambia chini ya ushauri pia wa taasisi za kidini zilivyofanya.
Haja yetu hapa ni kuwa na katiba mpya yenye Ibara na vifungu vinavyoainisha wazi haki na wajibu wa kila dini nchini. Na kuelekeza juu ya maingiliano na uhusiano mwema na adilifu kati ya dini hizo na kati ya dini hizo na makundi mengine ya kijamii ndani na nje ya nchi.
Tuzingatie kwamba kila dini ina haki na waumini wake wana haki wa kuabudu na kutekeleza ibada zao kwa mujibu ya mafundisho yao na kuwa na taasisi au vyombo vyote vile vitakavyosadia watu kuzifanya kamilifu ibada zao.
Katika hili, kwa kuwa wananchi wawezao kulipa kodi hulipa kodi na wao ni wa dini zote ni muhimu basi katika kuanzisha, kusimamia na kuendesha mambo yao ya kidini taasisi zote za kidini zipate msaada na ushirikiano sawa toka kwa viongozi wa kisiasa na serikali yao. Hili ni pamoja na serikali kuchangia pia katika kuwepo kwa Mahakama ya Kadhi na uendeshaji wake kama sehemu ambatanifu ya mfumo mzima wa 'Judiciary' au Mahakama na kuzingatia kwamba shauri lolote linaloamuliwa ama kisekula au kidini lina gharama fulani iliyostahili kulipwa na serikali inayochukua kodi toka kwa wananchi hao.
Jitayarisheni, jiandaeni na kujihami na nguvu za hoja kuhusu umuhimu wa kuwa na Baraza au Mkutano wa Kitaifa wa Katiba Mpya 2011 na wala sio Tume au Kikundi cha wateuliwa wachache hata kama ni mawaziri, wabunge, majaji, wanasheria na engineo kama hao, maana historia inaonesha wote hao hawawezi kutetea maslahi yako wewe na kwamba mwamba ngoma ngozi lazima avutie kwake au sio?
No comments:
Post a Comment