WANASHERIA siku yenu imefika. Siku ya kuhesabiwa. Je, mtakaa pembeni na kuachia maji yafuate mkondo wa kuishia kwenye maji mafu au mtaingilia kati na kuiona jamii inaelekezwa kwenye bahari ya Baraza la Katiba au Mkutano wa Kitaifa wa Katiba mpya 2o11. Nyie ni weledi na wajuzi zaidi kuliko mimi katika hili.
Sina ushauri wa ziada kwenu maana yote hapo juu yanayowahusu. Kwenu imebakia tu kuchagua mtaifuata njia gani. Njia itakayowafanya mkumbukwe na vizazi vijavyo kama mashuja au watu waoga na waliokosa sauti pale mlipohitajka kulisema kwa sauti kubwa lile lililopaswa kuzungumzwa na wakubwa wakalisikia.
Hii ni nafasi peke ya Majaji na wanasheria wetu kuhakikisha kuwa ile mihimili ya Kihistoria ya taifa, yaani, Serikali, Mahakama, Bunge na Vyombo vya Habari kama ilivyo kwa wenzetu huko Uingereza na Marekani kweli inakuwa huru na inayojitegemea na kushindana wakati huo huo kushirikiana ili kuiwezesha nchi hii kuwa mfano wa kuigwa katika Demokrasia na Haki za binadamu. Hili bila shaka litawafanya nyie Majaji, Mahakimu, mawakili na wanasheria wote kwa ujumla nchini kuwa mali katika soko la wanasheria Afrika na duniani kwa ujumla. Heshima hiyo mkipata Taifa letu litakuwa limeanza kwa kweli kuruka kama ndege tayari kuingia kwenye anga na kuelekea kule tunakotaka kwenda, yaani, kwenye demokrasia kamili na ya kweli na haki za kibinadamu za hali ya juu kabisa duniani.
Jitayarisheni, jiandaeni na kujihami na nguvu za hoja kuhusu umuhimu wa kuwa na Baraza au Mkutano wa Kitaifa wa Katiba Mpya 2011 na wala sio Tume au Kikundi cha wateuliwa wachache hata kama ni mawaziri, wabunge, majaji, wanasheria na engineo kama hao, maana historia inaonesha wote hao hawawezi kutetea maslahi yako wewe na kwamba mwamba ngoma ngozi lazima avutie kwake au sio?
http://www.blogger.com
No comments:
Post a Comment