MTANZANIA wewe ndiye unayemwajiri rais, mawaziri, wabunge na watumishi wa
umma. Na wewe ndiye mmiliki wa Katiba. Na katiba ni mchakato wa wewe
kuwaambia watawala waliopo na wajao unataka utawaliwe vipi na wao. Je, kuna
mtu mwingine anayeweza kuwasilisha ipasavyo unachokitaka kiwe, matakwa yako,
matarajio yako maslahi yako na ndoto ya Tanzania uitakayo na ile ya wewe
mwenyewe unachotaka kuwa kama sio mwakilishi wako anayeguswa na
yanayokugusa?
Hivi inawezekana sisi Watanzania tu wazito na wavivu kiasi cha kukosa hata
asilimia chache tu ya watu wetu wenye uwezo wa kuwa wabunifu na wavumbuzi
wa vitu, maarifa, mifumo na miundo mipya ya uendeshaji mambo ili kusaidia
kuharakisha maendeleo ya watu na nchi yetu ?
La, hasha. Soma magazeti na tazama televisheni utaona kuna wabunifu na
wavumbuzi wengi tu wa mambo mbalimbali. Ni serikali na wanasiasa ndio
walioshindwa kuandaa taasisi zenye mipango, mikakati, sera, muundo, mifumo
na watu wanaoweza kuchochea moto wa ubunifu na uvumbuzi badala ya kuuzima.
Wabunifu na wavumbuzi wote undeni kikundi cha dharura ili kuchagua watu wa
kuwasilisha madai, kilio na matakwa yenu mnayotaka yaangazwe katika katiba
mpya. Wakati ni huu, chelewa chelewa utamkuta mtoto si wako!
No comments:
Post a Comment