Thursday, May 26, 2011

47.. MTU WA KABILA AU ASILI FULANI.

JE, unajua wewe ndiye MMILIKI WA KATIBA na ndiye unayemwajiri rais, makamu wake, mawaziri na serikali nzima ?

Awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi hii ulianza kwa kukabili makabila na utamaduni wetu wa kila kabila kuzungumza lugha yake na wakati huo palikuwa na wengi waliokuwa hawajui Kiswahili bali wakizungumza lugha zao za kikabila.

Sababu kubwa iliyotolewa wakati huo ni kujenga umoja wa Kitaifa. Umoja huu kwa kiasi kikubwa umepatikana na tatizo hivi sasa sio ukabila ingawa huwezi kuuondoa kabisa maana kila mdhaifu katika kabila fulani hutaka kuutumia ukabila kuficha udhaifu wake. Hili wananchi wanalitambua na kama mahakama na vyombo vyetu vya sheria vinafanya kazi zake ipasavyo sio kitu kigumu kushguhulikiwa. Tishio letu sasa linaletwa zaidi na UKABILA WA KICHAMA (yaani watu wa chama kimoja tu wanapotawala na kushika vyeo vyote katika nchi husika); Udini kama tulivyoona hapo juu; Uongozi mbovu ; Upendeleo wa kimaeneo kutoka mawaziri wanakotoka; Ujinga na ubaradhuli wa baadhi ya watu wetu; Uporwaji wa maeneo yenye madini ya thamani bila wakazi wa asili kulipwa fidia muafaka; matumizi mabaya ya vyombo vya habari na hususan vile vya serikali vilivyosthili kuwa ni vyombo vya habari vya umma; na vyombo binafsi vinavyomilikiwa na wanasiasa au wapiga debre maprofeshenoo.

Inafaa kujiuliza maswali yafuatayo:
i. HIvi serikali na chama tawala vinataka lugha zetu za Kikabila, Kikwere, Kihaya,Kifipa, Kichaga, Kimasai na kadhalika kufa kwa faida ya Kiswahili?
ii. Je, Kiswahili kitakuwa na kuneemeka bila kuwepo kwa lugha za Kikabila ambako ndiko inakosemekana ni chimbuko la lugha hii katika makutaniko yake na lugha za nje?
iii. Kama watu wanazungumza kwa simu kwa kutumia Kikwere, Kijaluo au Kimasai au Kisukuma kwanini katika kuleta maendeleo ya haraka mikoani na wilayani pasiwe na redio zinazotumia lugha asili za maeneo hayokama UNESCO inavyopendekeza?
iv. Kwanini kila Kabila au Mkoa usiwe na majengo ya Makumbusho kwa kila kabila kama sehemu ya kutunza historia na utamaduni wetu kwa vizazi vijavyo na kwa manufaa yatakayoletwa na biashara ya Utali mjini na vijijini. Hivi ni sahihi kweli kuwa na jumba moja tu la makumbusho kama vile Watanzania wote wanatoka kwenye kabila moja?
v. Ni kwa namna gani urithi, ala na zana za kale za makabila yetu, lugha, nyimbo, ngoma, utamaduni, historia na jiografia yetu vinaweza lutengenenezwa kwa namna ambayo vinakuwa ni vivutio kwa wageni na hivyo kuyawezesha makabila mbalimabali na hususan vijijini kama wanavyofanya wenzetu Waganda na Wanyarwanda kuwa ni kivutio kwa watalii? Na hili likasaidia kupunguza umaskini ambao kwa hivi sasa ni sawa na mwendawazimu aliyekabidhiwa panga au jambia ?
vi Ni kwa namna gani kama serikali na wanasiasa kweli wana nia ya kuhafidhi lugha, mila na desturi zetu itachangia kuweka lugha zetu za asili mtandaoni ILI ZIISHI HUMO MILELE kwa kushirikiana na UNESCO, makampuni kama Microsoft, Google, Amazon na kadhalika;
vii. Ni kwa namna gani ili kuwatamanisha wageni toka nje kuja kutembelea makabila na vijiji vyetu tunaweza kuwa na namna fulani ya VIRTUAL MUSEUMS mtandaoni, yaani, wavuti zinazoonyesha kwa picha na video utamdauni na maisha ya kila siku ya watu wa kabila fulani baada ya kuboresha mambo kadhaa ili iwe ni sehemu ya kukuza Utalii Vijijini na Utalii wa Kijamii na wageni kukaa kwa wenyeji?

No comments:

Post a Comment