MAFUNDI wengi hawana kazi kwa sababu serikali, mipango na sera zilizopo zinawakwaza kwa mambo mengi tu.
Jiulize wewe fundi, mkeo na watoto wako mnaoishia mara nyingi kulala kwa njaa ila pale mpatapo maji ya kunywa au uji usio na sukari-hivi kama serikali ingelikuwa na mipango mizuri na programu ya UJENZI WA NYUMBA kwa familia zote za Kitanzania nchi nzima je, ungelilala na njaa au ungelikuwa katika neema?
Je, serikali ingelikuwa na mpango wa kujenga na kukarabati barabara zote VIJIJINI ewe ndugu Fundi Daudi hivi ungelikosa kuambulia chochote kila mwezi?
Hivi serikali ingelikuwa na mpango na mkakati wa kupatia watu umeme mijin na vijijini kwa haraka na kasi zaidi kuliko ilivyo sasa kwa mitambo midogo kwa mikubwa na kwa kutumia njia tofauti za vyanzo vya umeme, hivi kweli wewe ndugu yangu fundi umeme ungelikuwa hapo ulipo leo?
Na wewe mekanika, kama serikali ingekuwa imepanga maeneo ya kutosha kando au pembezoni ya miji yote na vijiji vyote nchini Tanzania kwa ajili ya magereji au maeneo ya kutengenezea magari, pikipiki, baiskeli, meli, ndege na kadhalika usingekuwa unakataa kazi kila wiki ?
Vitu hivi bwana wanasiasa wanaviongelea kuoga uoga na kijuujuu na wakishajua danganya toto yao itaonekana basi hutaka mara moja kukatiza mijadala na maandamano yanayotaka kuwafungua watu macho na masikio. Na sisi kwa uzawa na uzalendo wetu hili tunalikataa, mana mkifunguka macho ndio mwanzo wa mwisho wa utumwa kwa wanasiasa na viongozi wa nchi hii. Ndio mwanzo wa nyie kuanza kutwaa nafasi yenu kama wamiliki wa katiba na mabodi wa rais, mawaziri, wabunge na watumishi wote wa umma.
Ninakuambia hivi fundi, lazima na wewe pia uwemo kwenye Baraza au Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Katiba Mpya 2011.
Nchi yetu inathamini zaidi wawekezaji wenye asili ya kigeni kulikowa wazawa ambao ni wanadayaspora. Ni mlima kwa Wazawa wengi wanaotaka kuwekeza nyumbani au kujenga nyumba au kufanya hili au lile kwa sababu hata ndugu na wazazi wao wakati mwingine wameonesha kuwa laghai na kutokuaminika na wakiwaombea kifo ili wasirudi nyumbani na kukuta wamecheza mali ama fedha zao.
Lakini huko nyuma nikiandikia magazeti huru ya mwanzo Tanzania nilijaribu kuishawishi serikali kuzibadlli ofisi zetu za ubalozi kuwa ni vituo vya kiuchumi na kibiashara. Maendeleo ninayosikia yanayonesha kwamba wito huu umeitikiwa zaidi na wafanyakazi wenyewe kwenye balozi hizo lakini hili halifiki kwa Watanzania wasioko ubalozini kirahisi labda pale kunapokuwa na viungo vya undugu na urafiki na baadhi ya watu ubalozini.
Mwanadayaspora (diaspora) hivi nani atakayezitoa dukuduku zako zote hizo hapo juu na zingine ambazo nimemezea na hasa inapokuja kwa wanafunzi wa Kitanzania walioko nchi za nje na wajasiriamali wanaotafuta mwanya wa wao kujijenga na kuwa wafanyabiashara wa kimataifa ?
No comments:
Post a Comment